Makamu wa Rais kuongoza wanariadha mbio za Mazingira marathoni

Monday October 25 2021
mbio pic
By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango atawaongoza wanariadha zaidi ya 2000 kwenye mbio ya Mazingira marathoni itakayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.

Wanariadha wa ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kukimbia kwenye mbio hiyo ya Novemba 14 itakayoanzia na kumalizikia kwenye viwanja vya Farasi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa mbio hiyo, Amon Mkoga amesema jana kwa mbio hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhifadhi mazingira nchini.

Amesema wanariadha watachuana katika mbio za nusu marathoni (kilomita 21), kilomita 10 na kilomita tano ambayo makamu wa rais pia atakimbia mbio hiyo.

"Maandalizi yameanza kwa wakimbiaji kujiandikisha kwa njia ya mtandao, mbio hii mbali na kuhamasisha utunzaji wa mazingira ambao utakwenda sanjari na upandaji miti, pia utasaidia vifaa vya uzazi kwa wa kina mama.

"Katika utoaji vifaa, tunashirikiana na Tasaf na vifaa hivi vitatolewa kwa kaya masikini kwenye maeneo mbalimbali nchini," amesema.

Advertisement

Mmoja wa wasanii kwenye mbio hiyo, Haruna Kahena 'Inspector Haroun' ambaye ni miongoni mwa watakaokimbia mbio za kilomita 5 alisema anatamani mabingwa wote watoke nchini.

Amesema mbali na mbio hiyo kuwashindanisha wakimbiaji nyota nchini, lakini pia ni sehemu ya mazoezi kwa wengine na kuwashauri watu kujitokeza kwa wingi kushiriki.

Advertisement