MAJONZI : Mastaa wanavyomlilia Kobe Bryant

Muktasari:
Bryant, bingwa mara tano wa NBA, aliitumikia LA Lakers kwa maisha yake yote ya mchezo wa kikapu na kuhesabika kama mmoja wa wachezaji waliofanya makubwa kwenye historia ya mchezo huo.
CALIFORNIA , MAREKANI . GWIJI wa mpira wa kikapu, Kobe Bryant na moja ya mabinti zake walikuwa miongoni mwa watu tisa walioawa kwenye ajali juzi Jumapili wakati helikopta yao ilipogonga mlima huko Calabasas, California, imeelezwa.
Bryant, 41, na binti yake mwenye umri wa miaka 13, Gianna Maria Onore Bryant walikuwa kwenye msafara kwenda kwenye akademia ya Mamba Sports huko Thousand Oaks kwenye mechi ya kikapu iliyopangwa kufanyika juzi.
Gianna alitarajia kucheza kwenye mchezo huo na Bryant alitarajia kuwa kocha kwa mujibu wa mkurugenzi wa timu ya Lady Mavericks, Evelyn Morales. Helikopta hiyo iligonga mwinuko huo maili 30 Kaskazini Magharibi mwa Los Angeles na kulipuka imetoa taarifa mamlaka ya zima moto ya Los Angeles kupitia bosi wake, Daryl Osby. Watu tisa walipoteza maisha yake kwenye ajali hiyo.
Bryant, bingwa mara tano wa NBA, aliitumikia LA Lakers kwa maisha yake yote ya mchezo wa kikapu na kuhesabika kama mmoja wa wachezaji waliofanya makubwa kwenye historia ya mchezo huo.
Kwanini Kobe alikuwa maarufu?
Alizaliwa Philadelphia, Bryant alianza kucheza kikapu tangu akiwa na umri wa miaka mitatu kabla ya kuja kuwa staa mkubwa kwenye NBA. Alipandishwa kutokea Shule ya Lower Merion High School iliyopo karibu na Philadelphia mwaka 1996. Alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza NBA katika kistoria ya mchezo huo, alipocheza akiwa na umri wa miaka 18 miezi miwili na siku 11.
Bryant kwa miaka yake yote 20 aliyocheza kwenye kikosi cha Los Angeles Lakers. Alistaafu Aprili 2016.
Mafanikio yake makubwa ikiwamo kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa NBA (MVP) mwaka 2008 (MVP) na kuchaguliwa MVP mara mbili kwenye fainali ya NBA. Alikuwa mfungaji bora wa mabingwa wa NBA mara mbili na alishinda ubingwa wa Olimpiki mara mbili.
Umaarufu zaidi ilikuja alipowafunga pointi 81 Toronto Raptors mwaka 2006, akiweka rekodi ya kuwa mtu wa pili kufunga pointi nyingi kwenye mechi moja katika historia ya NBA. Alishinda pia Oscar baada ya filamu yake ya mwaka 2018 ya Dear Basketball, filamu ya dakika tano iliyozungumzia barua ya mapenzi kwenye mchezo huo aliyoandika mwaka 2015. Kuhusu familia, Bryant na mkewe mrembo Vanessa, watoto wao wengine watatu ambao pia ni wa kike Natalia, Bianca na Capri.
Kupenda helikopta
Miaka 10 iliyopita, Jarida la GQ liliandika namna Bryant anavyopenda usafiri wa helikopta, ambao ndio amekuwa akiutumia kama usafiri wake wa kutoka nyumbani kwenda kazini kila siku. Kutokana na hilo huko nyuma kuna mtu aliwahi kusema kwamba kuna uwezekano wa staa huyo akaja kufariki kwenye ajali ya helikopta, kutokana na mapenzi yake na usafiri huo na kitu hicho ndicho kilichokuja kutokea.
Msiba wake washtua
Taarifa za kifo cha staa huyo zimewashtua wengi na kuweka wazi hisia zao juu ya gwiji huyo wa kikapu.
Shaquille O’Neal, aliyecheza na Bryant huko Lakers kati ya mwaka 1996 na 2004, alisema: “Hakuna maneno yanayofaa kuzungumzia maumivu haya ninayopitia kwa sasa. Nakupenda na daima nitakukumbuka,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kisha akaweza picha ya pamoja wakiwa na jezi za Lakers.
Deron Williams, ambaye alishinda medali ya dhahabu kwenye Olimpiki sambamba na Bryant, alisema kinywa chake kimekuwa kizito, lakini alimwelezea marehemu kama mtu aliyekuwa mshindani wake mkubwa na ilikuwa bora zaidi kucheza timu moja.
Staa wa zamani wa kikapu Tony Parker alisema: “Moyo umevunjika”.
“Habari mbaya,” aliandika Rais wa Marekani, Donald Trump kwenye Twitter. “Alipenda sana familia yake na alikuwa na mapenzi makubwa ya hatima yao. Kufariki kwa binti yake mrembo Gianna, hili linaumiza zaidi.”
Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama alimzungumzia Bryant kuwa ni gwiji kwenye uwanja wa mpira wa kikapu. Staa kwenye riadhaa na mshindi wa medali ya dhahabu kwenye Olimpiki, Usain Bolt alisema awali hakuwa akiziamini taarifa hizo za kifo, huku Rapa Kanye West akishukuru kila kitu alichokifanya kwenye maisha yake aliyokuwa akiishi kwamba yamewaachia kitu cha kujifunza.
Wanasoka maarufu wamlilia
Supastaa wa Kibrazili, Neymar alifunga bao tu dhidi ya Lille alichagua kushangilia kwa kumkumbuka gwiji huyo wa mpira wa kikapu. Neymar, ambaye ni mpenzi mkubwa wa mpira wa kikapu aliwahi kukutana na Bryant katika enzi za uhai wake, hivyo alipofunga tu bao, alishangilia kwa kunyoosha vidole juu kama kumbukumbu ya waliotangulia mbinguni.
Fowadi wa Manchester City, Raheem Sterling aliandika: “Pumzika kwa amani gwiji” kupitia Twitter kisha akaweka picha yenye rangi nyeusi na nyeupe inayomhusu staa huyo.
Masupastaa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ni miongoni mwa mastaa wengine wakubwa kwenye soka walioguswa na msiba huo wa Bryant. Staa wa Barcelona Messi, aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram, alise: “Nimeishiwa maneno…naelekeza pole zangu kwa familia ya Kobe na marafiki. Ilikuwa furaha kukutana na wewe na kushiriki nyakati nzuri pamoja. Ulikuwa jiniazi kama walivyo wengine wachache.”
Staa wa Juventus, Ronaldo aliandika kwenye Twitter: “Inauma sana kushikia taarifa hizo zinazovunja moyo zinazowahusu Kobe na binti yake Gianna. Kobe alikuwa gwiji wa kweli na amewahamasisha wengi. Natuma rambirambi zangu kwa familia na marafiki na wanandugu waliopoteza watu wao katika ajali hiyo. Pumzika kwa amani gwiji.”
Straika wa Inter Milan, Romelu Lukaku aliandika: “Shujaa wangu mkubwa kwenye michezo. Utendaji wako kali na akili ya mchezo zilinipa ujasiri wa kupambana. Nakupenda sana bingwa.”
Beki wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk alisema: “Nimeishiwa maneno, moyo umevunjika pia!”