Majeruhi Bayern waibana Dortmund, Pep ashangilia bao sekunde mbili tu
Muktasari:
Hadi timu zikikaribia katika dakika za nyongeza hakukuwa na bao ingawa hadi hapo juhudi zilizoonekana kwa upande wa Dortmund zilikuwa ni mbili ambazo zilileta misukosuko langoni mwa Bayern ukiwamo mpira wa kichwa uliopigwa na Hummels.
TOLEO lililopita kwenye kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau alizungumzia jinsi Kocha Pep Guardiola alivyompa winga Franck Ribery majukumu mapya katika mechi na Dortmund kutokana na janga la wachezaji majeruhi katika kikosi chake. Endelea…
Pep naye akaamua kuwabadili nafasi Ribery na Gotze, maana yake, Kroos akawa karibu na Gotze, wakiwa eneo la kati mbele ya mabeki wa kati.
Alichotaka Pep ni kuona Ribery analisogelea zaidi lango la Dortmund ingawa hiyo pia maana yake, Ribery alikuwa anatolewa eneo ambalo tayari alianza kuonyesha uwezo.
Hummels aliunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ambao ulimpita Neuer na kuonekana ukienda wavuni lakini Dante aliuwahi ingawa ilionekana kama mpira ulikuwa umejaa wavuni lakini mwamuzi alisema halikuwa bao.
Hadi timu zikikaribia katika dakika za nyongeza hakukuwa na bao ingawa hadi hapo juhudi zilizoonekana kwa upande wa Dortmund zilikuwa ni mbili ambazo zilileta misukosuko langoni mwa Bayern ukiwamo mpira wa kichwa uliopigwa na Hummels.
Bayern walicheza kwa uangalifu na umakini mkubwa na katika lango la wapinzani wao, walifanya mashambulizi matano ikiwamo kuwadhibiti Dortmund katika silaha au sifa yao kubwa yaani mashambulizi ya kushtukiza.
Wakati wa mazungumzo ya mapumziko kabla ya kuingia uwanjani kwa dakika za nyongeza, Pep akawakumbusha wachezaji wake wanaingia katika hatua ambayo akili na fikra zao zinatakiwa kusimamia kila kitu badala ya miguu pekee, msisitizo wake hapo ulikuwa katika umakini, kujiamini na kuwa na dhamira ya kusaka ushindi.
Mwishowe hakuwa na maelekezo mengi bali aliwaambia, “Mwangalieni Mario (Gotze) mpeni mipira katika maeneo sahihi.
Kwa upande mwingine, Ribery naye alikuwa katika hatua za mwisho, maumivu ya mgongo yalimzidia na Pep na Robben wakaanza kujadiliana suluhisho la tatizo hilo.
“Pep aliniuliza kama ningeweza kuendelea.” Mholanzi huyu aliniambia kesho yake.
“Nilimwambia ndio, lakini nilimwona Ribery alikuwa na wakati mgumu na asingeweza kuendelea wakati huo huo Hojbjerg naye alipata matatizo ya misuli, tulitakiwa kuendesha jahazi katika ubora kwa kadri ambavyo ingewezekana.”
Kama ambavyo Pep alishauri, dakika za nyongeza baada ya matokeo kuwa sare ni suala la nguvu za akili na si nguvu za mwili pekee na kwa kawaida inapofikia muda kama huo wachezaji walio wengi miguu inakuwa imechoka wameishiwa nguvu na hapo ndipo mambo yanapoanza kuwa mabaya.
Haikuchukua muda baada tu ya kupasha na kuingia uwanjani kwa hatua hii ngumu ya mpambano mkali wa dakika za nyongeza, Kroos akafanya kosa lake la kwanza, akamruhusu Aubameyang apate nafasi ya kufumua shuti.
Kutokana na utelezi uliokuwa uwanjani ulimfanya Neuer ateleze na kuangukia bega la kulia ambalo liliumia. Neuer aliendelea na mchezo lakini kwa kipindi chote cha dakika 30, alimalizia mchezo begani akiwa amewekewa barafu eneo aliloumia.
Kilichofuata baada ya hapo ni majanga mengine kwa Kroos akatonesha misuli iliyokuwa ikimsumbua hali iliyomfanya acheze akiwa mwenye kuchechemea kwa dakika zote 30.
Muller naye alikuwa na matatizo yanayofanana na hayo lakini kwa Hojbjerg hali ilikuwa mbaya zaidi hadi kocha akaamua kumpumzisha na nafasi yake kuchukuliwa na Van Buyten.
Pamoja na mazingira yote hayo, Bayern bado ilijitahidi na kucheza mpira kwa kuanzia nyuma na kufika eneo la timu pinzani, muunganiko mzuri kati ya Martinez na Kroos ulisaidia kufanikisha hilo na zaidi ya yote, bado Dortmund walibanwa na kushindwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo ni moja ya sifa ya timu hiyo.
Pizarro naye alianza kupasha, alikuwa akijiandaa kuchukua nafasi ya Ribery na hapo hapo bao likapatikana, Boateng alitoa pasi ndefu iliyonaswa na Ribery aliyempasia Robben ambaye aliambaa nao kwa kasi kwenda eneo la penalti na kufumua shuti.
Kipa wa Dortmund, Weidenfeller akauzuia na mpira kwenda kwa beki wake Kevin Grosskreutz lakini Boateng akaunyakua mpira kwa beki huyo wa Dortmund na kumpasia Robben ambaye akasababisha majanga kwa Dortmund.
Baada ya kupata bao, furaha ya Pep ilidumu kwa sekunde kama mbili hivi, baada ya hapo fikra zake zikarudi katika mpango wake wa kumweka benchi Ribery kwa sababu hadi hapo tayari alionekana dhahiri akiwa mwenye kuchechemea.
Itaendelea Jumamosi ijayo…