Majembe mawili yampa jeuri Nabi Yanga

Tuesday October 12 2021
nabi pic
By Khatimu Naheka
By Thomas Ng'itu

HUKU Jangwani mashabiki wa Yanga wamepokea taarifa njema za kurejea kwa mabeki wao wawili waliokuwa wamekaa nje kwa muda mrefu na salamu hizo zikamfanya Kocha wao Nesreddine Nabi kutamka kwa sasa presha yake imeshuka na anatengeneza kikosi kitakachowapa raha mashabiki wake.

Yanga ambayo ilivaana na JKU ya Zanzibar katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa imetoka kuwapokea mabeki wake Yasin Mustafa aliyekuwa majeruhi wa muda mrefu tangu msimu uliopita lakini utamu zaidi kuna beki wao mpya wa upande huo huo wa kushoto David Bryson naye amerejea.

Bryson aliyesajiliwa kutoka KMC, hajawahi kucheza mchezo wowote mkubwa na kuonekana kwa mashabiki wa timu hiyo zaidi ya kucheza mechi za kirafiki tu kule Avic zinazoshuhudiwa tu na mabosi wa klabu hiyo.

Hata hivyo, mabeki hao sasa wameanza kufanya mazoezi ya nguvu na wenzao wakiwa kamili gado lakini mwenye uhakika zaidi Mwanaspoti linafahamu ni Bryson ambaye atawahi kuanza hiyo akimtangulia Mustafa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Nabi alisema amefurahi kurejea kwa mabeki hao na sasa wanakwenda kuimarisha upande wa beki ya kushoto uliokuwa ukilindwa kwa mechi za karibuni na beki wa kulia Kibwana Shomary.

Nabi alisema alikuwa hataki kufanya haraka kumpa nafasi Bryson kutokana na kutokumaliza programu maalum aliyotaka aipitie kabla ya kuanza mechi za ushindani.

Advertisement

Aliongeza, Bryson ni beki bora ambaye atakwenda kuleta ushindani mkubwa upande wa kushoto akithibitisha hilo katika mechi za kirafiki alizocheza akiwa na Yanga.

“Mashabiki wengi walikuwa wanadhani mimi sitaki kumchezesha Bryson lakini sikutaka kumuumiza zaidi alitakiwa kupitia hatua mbalimbali ili awe sawa kucheza mechi za ushindani,” alisema Nabi na kuongeza;

“Nimemwona katika mechi zetu za huku, ni beki mzuri atakayekuja kushindana vizuri na wenzake Yassin na hata Adeyun (Saleh) upande wa kushoto.”

Tangu kuumia kwa mabeki hao wawili, Nabi alilazimika kumtumia sana Adeyun upande huo ingawa hivi karibuni katika mechi za Ligi Kuu amelazimika kumhamisha Kibwana kucheza upande huo wa kushoto.

Mshambuliaji wa zamani Yanga, Herry Morris alisema urejeo wa Mustafa ni jambo zuri lakini kutakuwa na vita ya kuwania namba.

Morris alisema Bryson (David) ni mzuri na alikuwa akimfuatilia akiwa kwenye kikosi cha KMC hivyo uwezo atakaouonyesha Yanga pia utampa nafasi ya yeye kucheza.

“Mustafa amerejea ila bado hajawa fiti kucheza moja kwa moja, japo sijamuona ila kiuhalisia lazima iwe hivyo na yeye atakuwa na uoga wa kuumia, wanatakiwa wawe kwenye kiwango kizuri cha kupiga krosi kwani ndio tulichokikosa kwa sasa;” alisema.

Naye kocha wa zamani Yanga, Kenny Mwaisabula alisema urejeo wa Mustafa ni kitu kikubwa kwa Yanga kwa sababu ni beki ambaye ana uwezo mkubwa wa kucheza na mguu wa kushoto.

“Namfahamu vizuri Yassin na anajua kushambulia huku silaha yake kubwa ikiwa ni krosi zake za mguu wa kushoto, Kibwana anatakiwa ajiangalie kwa sababu yeye kule sio namba yake alienda kusaidia,” alisema Mwaisabula.

Advertisement