Mafans walitii ili mambo yaishe tu

Muktasari:

Mashabiki wa soka na michezo mingine hawakuwa na jambo la zaidi kwani, walifuata maelekezo ya serikali ya kuwataka kusalia majumbani ili kudhibiti maambukizi ya corona.

MLIPUKO wa virusi hatari vya corona uliotua nchini Mwezi Machi 2020 ulivuruga shughuli za michezo na kuchangia mengi kinyume na matarajio ya wengi. Ligi zote zilipigwa breki na maamuzi yaliyofuata yalichangia furaha pia malalamishi kwa baadhi ya wahusika.

Mwanzo wa ngoma Gor Mahia  ilitangazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kwa mara ya 19 bila kushiriki mechi zote msimu huo.

Uamuzi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ilipotangaza K’ogalo mabingwa ulichangia wasimamizi wa KPL kuekelea katika mahakama ya kutatua Mizozo ya Vyama vya Michezo Nchini (SDT) kupiga tangazo hilo ambalo mwanzo lilitolewa na Rais ,Nick Mwendwa kupitia mtandao wa Twitter.

Gor Mahia chini ya kocha, Steve Palock ilitangazwa bingwa kwa alama 39, tano mbele ya Tusker FC baada ya kushiriki mechi 16. Nayo Kakamega Homeboyz iliokuwa ikipigiwa chapuo kubeba ubingwa wa msimu huo ilimaliza ya tatu kwa alama 33.

 SHIMANYULA

Hatua hiyo ilichangia malalamishi kibao kutoka kwa bosi wa Kakamega Cleophas ‘Toto’ Shimanyula kati ya wengine. Shimanyula alinukuliwa akisema ‘’Gor Mahia ilipendelewa kutuzwa taji hilo pia Mwendwa alichukua uamuzi huo kusudi asaidie klabu yake Kariobangi Sharks isiteremshwa ngazi.’’

 Bosi huyo alisema wangeshiriki mechi zote Gor Mahia ingeambulia patupu haingepata ubingwa huo.

Klabu nyingi zilizua malalamishi huku zikidai Mwendwa alitangaza Gor Mahia mabingwa kwenye juhudi za kujitafutia kura ya klabu hiyo.

SAJILI WAPYA

 Gor Mahia ilikuwa na ushindani mkali kutoka kwa Kakamega Homeboyz, Tusker FC, KCB, Western Stima, Ulinzi Stars bila kusahau AFC Leopards. Licha ya kufanya wahusika wengi katika soka kujikuta njia panda hasa kukosa namna ya kujipatia kipato hatua ya michezo kusitishwa ilichangia wasimamizi wa klabu mbalimbali kuwazia namna ya kuboresha vikosi vyao.

Katika kipindi hiki cha usajili K’Ogalo inajivunia kunasa sajili kumi wapya baada ya kupoteza takribani wanasoka saba akiwamo Lawrence Juma aliyenaswa na Sofapaka FC, Joash Onyango (Simba FC), mnyakaji David Mapigano (Azam FC), winga Dickson Ambundo (Dodoma Jiji) za Tanzania pia Boniface Omondi na kipa Peter Odhiambo wote Wazito FC ya Kenya. 

Gor Mahia imenasa vifaa vipya kama Benson Omalla, Mburundi Jules Ulimwengu, Mganda Tito Okello, Dickson Raila, John Macharia na  Andrew Malisero Numero raia wa Malawi kati ya wengine. Nayo AFC Leopards maarufu Ingwe ambayo hadi sasa haijatangaza wanasoka iliyosajili ilipoteza wachezaji kadhaa huku Wazito FC ikiachia wapigagozi 12 na kusajili idadi karibu na hiyo tayari kujiweka fiti kwa kampeni za muhula ujao.

TATU ZAKOSA MDHAMINI

Ni ndani ya kipindi hiki ambapo klabu tatu: Western Stima, Nairobi Stima na Coast Stima zimepoteza mdhamini wao kampuni ya Umeme ya (KPLC). Kampuni hiyo ilisitisha ufadhili wake kwa vikosi hivyo ikilalamikia kudorora kwa biashara yake hali iliyochangiwa na janga hilo. Kufuatia hatua hiyo hadi sasa haijulikana kama klabu hizo zitashiriki kampeni za msimu ujao.

Kwa washiriki wa kipute cha Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL), ingawa Nairobi City Stars ilikuwa ikifanya kweli mlipuko huo ulichangia kutangazwa bingwa bila kucheza mechi zote. City Stars maarufu Simba wa Nairobi na Bidco United kila moja ilitangazwa kuzoa tiketi ya kufuzu kushiriki kipute cha Ligi Kuu muhula ujao.

Pia hatua ya kumaliza ligi zote kabla ya klabu husika kushiriki mechi zote ilizua malalamishi chungu mzima huku baadhi ya timu zilizoshushwa ngazi zikitaja zingeshiriki mechi zote zingetia bora na kukwepa shoka hilo.

Kadhalika kuibuka na virusi hivyo kulichangia Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuhairisha michuano ya kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (afcon) 2012. Mechi hizo zilizokuwa zimepangwa kuchezwa mwezi Machi 2020 sasa zimepangwa kugaragazwa mwezi Novemba.