Machezo kumrithi Mkude Simba

Dodoma. Simba inakaribia kumalizana na kiungo wa Mbeya City, Hassan Maulid Machezo 'Rasta' kwa ajili ya kuziba pengo la Jonas Mkude, ambaye inadaiwa uongozi wa klabu hiyo unapanga kuachana naye mwisho wa msimu huu.

Machezo amekuwa sehemu ya wachezaji wanaoanzishwa na kocha Abdallah Mubiru na amekuwa msaada mkubwa msimu huu akishirikiana na Sixtus Sabilo, Juma Shemvuni na Davis Mwasa.

Kiungo huyo ambaye amewahi kuzichezea KMC na Dodoma Jiji amekuwa akimudu kucheza kama kiungo mkabaji (namba 6), mchezeshaji (namba 8) pamoja na namba 10.

Machezo ni sehemu ya wachezaji wa timu ya Taifa ya  Tanzania chini ya miaka 23, Ngorongoro Herous.

Mmoja wa marafiki wa mchezaji huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema tayari uongozi wa Simba umemfuata mchezaji huyo na baadhi ya mambo yamekaa sawa na kinachosubiriwa ni kusaini mkataba.

“Nimecheza naye Dodoma Jiji hata kwenda Mbeya City, mimi ndiyo nilimshauri aende, amenieleza kila kitu, kinachosubiriwa sasa ni kusaini tu mkataba,” alisema.

Kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' alishawapa uongozi wa Simba majina ya wachezaji anaowahitaji kwenye kikosi chake msimu ujao na moja ya mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni alikiri hilo.

"Nahitaji kila nafasi iwe na ushindani, anayeingia na kutoka wafanye kazi sawa, tayari viongozi nimewapa ripoti ya nini nakihitaji naamini wanaifanyia kazi kikamilifu," alisema Oliveira.

Kwa upande wake, Machezo alisema: "Mimi natafuta maisha, nipo tayari kucheza popote, ila tusubiri kwanza tumalizie mechi zilizobaki nitakuwa katika sehemu nzuri ya kulizungumzia hili.

"Umekuwa msimu bora kwangu na natamani kutafuta changamoto nyingine ili kukiendeleza kipaji changu," alisema kiungo huyo.