Maafande watoshana nguvu Ligi Kuu

Muktasari:

Mchezo wa timu za jeshi umemalizika kwa sare ya 1-1 mchezo uliopoigwa leo saa 8:00 mchana katika uwanja wa Ushirika, Moshi.

TIMU za jeshi la Polisi Tanzania na JKT Tanzania zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa leo Ijumaa mchana katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Katika mchezo huo Polisi Tanzania ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika 34 kwa mpira wa adhabu baada ya beki wa JKT kuunawa na  Daruesh Saliboko alipiga shuti la chini chini na kwenda wavuni.

Licha ya JKT Tanzania kuwa nyuma hawaonyesha kukata tamaa badala yake walikuwa wanapambana muda wote kuhakikisha wanasawazisha na kupata bao la nyongeza.

Bao hilo lilidumu katika kipindi cha kwanza ambapo JKT Tanzania walishindwa kusawazisha na kufanya mchezo kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao moja.

Kipindi cha pili JKT Tanzania walianza kwa kasi wakionyesha kuhitaji bao, ambapo dakika 63 mshambuliaji Kelvin Sabato aliisawazishia timu yake kwa kuunganisha krosi ya Michael Aidan kwa kichwa na mpira kwenda moja kwa moja wavuni huku kipa akiwa hajui nini cha kufanya.

Bao hilo liliwarejesha JKT Tanzania mchezoni na kufanya mechi hiyo kuwa na utulivu kwa timu zote huku kila mmoja kupata bao la kuongoza lakini mpaka mpira unaenda mapumziko hakuna aliyeongeza bao.

Kwa matokeo hayo yanawafanya timu zote kugawana pointi moja moja na kila timu kufikisha pointi nne.