Maafande wafunika shindano kula matikiti

ASKARI wa Jeshi la Uhamiaji, Koplo Emmanuel Shayo na Koplo Sara Nambarara wameibuka washindi wa shindano la kula tunda la tikiti maji wakiwafunika wapinzani kutoka Morogoro katika Tamasha maalumu la Bonanza la Nyerere Day lililofanyika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Kiislam (Mum) mjini Morogoro.

Washindi hao kila mmoja waliwashinda wapinzani wao kwa kula kipande cha tikiti ndani ya sekunde 30, tikiti lenye uzito wa nusu kilo na kugawanywa vipande vinne na kila mshiriki kula kwa muda uliopangwa.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Koplo Sara alisema ana mbinu nyingi za kula tikiti na moja iliyompa ushindi ni kumega kipande cha tikiti kwa meno na kumeza bila kutafuna jambo ambalo wapinzani wake hawakuweza kugundua mbinu hiyo kumpatia ushindi.

“Michezo hii midogo imetuchangamsha akili na askari siku zote anapaswa ujiongeze kutafuta mbinu ya kupambana na vikwazo, kwangu shindano hili ilinilazimu kumeza kipande cha tikiti bila kutafuta na mbinu hii ilinisaidia kushinda hata afande Shayo alitumia mbinu hiyo kushinda mpinzani wake wa Morogoro,” alisema.

Mratibu wa bonanza hilo, Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Morogoro, Vicent Haule alisema lengo la kuwakutanisha askari hao ni kuadhimisha kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwl Julius Nyerere kwa kucheza michezo na kubadilisha uzoefu wa kazi katika jeshi hilo.

Kamanda Haule alisema askari zaidi ya 60 kutoka Dar es Salaam wameshiriki michezo ya soka, netiboli, riadha, mbio za magunia, kufukuza kuku, kukimbia na mayai na kula vipande vya tikiti.

Katika mchezo wa soka, Uhamiaji Dar es Salaam iliibuka na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Morogoro wakati netiboli Uhamiaji Morogoro iliwalaza wenzao wa Dar es Salaam kwa vikapu 17-1.