Lyanga awapa presha mashabiki wao

Muktasari:


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati Coastal ikifanya mazoezi yake, mashabiki hao walionyesha kulalamika kukosekana kwa mchezaji huyo anayeonekana kuwa tegemeo kikosini kwamba kunaweza kuathiri kikosi chao.

KUTOONEKANA kwa winga wa kulia wa Coastal Union, Ayoub Lyanga kwenye mazoezi yaliyofanyika Mkwakwani kwa siku mbili jana Ijumaa na  leo Jumamosi kumewapa hofu wapenzi wa timu hiyo jijini hapa kuhusu hatma ya mchezo wao wa kesho Jumapili dhidi ya Yanga.

Coastal Union wanaikaribisha Yanga kesho Jumapili uwanja wa Mkwakwani ikiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati Coastal ikifanya mazoezi yake, mashabiki hao walionyesha kulalamika kukosekana kwa mchezaji huyo anayeonekana kuwa tegemeo kikosini kwamba kunaweza kuathiri kikosi chao.

“Kwanini Lyanga hayupo uwanjani? isijekuwa ni njama ili tufungwe na Yanga tunamuuliza kocha Juma Mgunda hatuelezi chochote," alisema Sufian Bakari mkazi wa Ngamiani
Nurdini Omar  alisema kutokuwepo kwenye mazoezi mchezaji huyo kunawatia wasiwasi mashabiki kuhusu mechi baina yao na Yanga.

Mgunda alisema Lyanga hakuonekana mazoezini kwa siku hizo kutokana na maagizo ya daktari wa timu hiyo, Kitambi Mganga kumtaka apumzishwe kwanza.

Alisema Lyanga alipata majeraha wakati wa mechi baina ya Coastal Union na Ruvu Shooting ambapo aliumizwa mapajani hivyo daktari alimpa mapumziko ingawa mechi ya kesho atakuwepo kikosini.

“Mashabiki wetu waje kwa wingi kwa sababu Lyanga atacheza kama kawaida na tutapambana ili kupata alama tatu muhimu, alipumzishwa kutokana na ushauri wa daktari baada ya kuumia,” alisema Mgunda.