Ligi ya Kabaddi Zanzibar imenoga
Muktasari:
- Katika mizunguko miwili iliyochezwa ya ligi hiyo, KMKM imefanikiwa kushinda mechi mbili kwa pointi 101, huku Nyuki nayo ikishinda miwili kwa kukusanya pointi 84.
LIGI ya Kabaddi Zanzibar msimu wa pili imeanza kushika kasi huku timu ya KMKM kwa upande wa wanaume wanaongoza wakifuatiwa na Nyuki baada ya kila moja kucheza mechi mbili.
Katika mizunguko miwili iliyochezwa ya ligi hiyo, KMKM imefanikiwa kushinda mechi mbili kwa pointi 101, huku Nyuki nayo ikishinda miwili kwa kukusanya pointi 84.
Kocha wa KMKM, Tamajiha Saburi, amesema wameridhika na ushindi huo na watajiandaa vizuri ili kutwaa ubingwa.
"Wapinzani wetu tumewazidi kwenye utulivu na uzoefu ndio sababu ya kufanya vizuri," amesema Saburi.
Wakati VTA Kabaddi iliyokuwa inaongoza msimamo awali kwa pointi 94 imeshuswa hadi nafasi ya tatu baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya KMKM walioibuka na ushindi wa pointi 42-29, ambapo sasa ina pointi 96.
Timu ya Fighetrs Kabaddi inashikilia nafasi ya nne ya msimamo huo baada ya kupoteza mechi moja dhidi ya Deaf na kufanikiwa kuvuna pointi 70.
Katika msimamo huo, timu ya Deaf ipo nafasi ya tano kwa kupoteza mechi zote huku ikikusanya pointi 45 kwenye michezo hiyo na JKU ipo nafasi ya sita ikiwa na jumla ya pointi 30.
Kwa upande wa wanawake, timu ya Nyuki Kabaddi ipo nafasi ya kwanza baada ya kutoa sare 32-32 dhidi ya JKU iliyopo nafasi ya pili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa JKU, Asha Khamis, amesema sababu kubwa ambayo imewafanya kuwa mwisho wa msimamo huo ni uchanga ulionao timu hiyo.
Amesema, kwasasa timu hiyo inahitaji mazoezi ya hali ya juu ili kuwa bora zaidi ya wengine huku akibainisha kwamba ligi hiyo ni sehemu ya mazoezi kwao.