KVZ wapewa mchongo CAF

KVZ wapewa mchongo CAF

KVZ inatarajiwa kufungua pazia kwa timu za Tanzania kwenye michuano ya Afrika ikiwa ugenini nchini Sudan na katika kuhakikisha inaanza na mguu mzuri, Kocha wa Malindi, Mohammed  Badru amewapa mchongo wa maana na kama watautumia lazima watoboe.
Kikosi hicho kutoka Zanzibar, kitakata utepe wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Amal Atbara na Badru ambaye ni mdogo wa kocha wa zamani wa Taifa Stars, Hafidh Badru alisema anaifahamu vizuri KVZ na kwa muda ambao amewasoma wapinzani wao ni vema wachezaji watambue kuwa wanakazi kubwa mbele yao.
"Aina ya mpira wetu kiasili ni ngumu kucheza kwa kuzuia lakini muda mwingine inapobidi basi hakuna jinsi kwa sababu hizi ni mechi za mahesabu. Jambo muhimu ni jihadi wakumbuke Wazanzibar na Watanzania wote wapo nyuma yao," alisema kocha huyo.
Mchezo wa marudiano baina ya KVZ dhidi ya  Al Amal Atbara, unatarajiwa kuchezwa, Desemba 4 visiwani Zanzibar na mshindi wa mchezo huo ataingia raundi ya kwanza ambapo atakutana na ushindi wa jumla ya mchezo kati ya  Ashanti Gold ya Ghana dhidi ya  Salitas ya Burkina Faso.
Mara baada ya KVZ  kucheza Ijumaa, wawakilishi wengine wa Zanzibar, Mlandege  watakuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na Watunisia, CS Sfaxien  katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa Tanzania Bara, Namungo ambao ni wawakilishi wa Kombe la Shirikisho itaikaribisha Al Rabita ya Sudan Kusini, Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex huku  Simba kwenye Ligi ya Mabingwa ipo ugenini Nigeria kupepetana na Plateau United, Jumapili.

___________________________________________________________________

Na ELIYA SOLOMON