Kuna sababu nyingi za kumpenda Ronaldo

Muktasari:

Mashabiki kibao wamekuwa wakimpenda kwa soka lake, lakini mwenye mafanikio hakosi pia wanaomkosoa, na ndio maana Mreno huyo ni moja ya wakali wasiopendwa pia ndani ya uwanja, wakitazamwa kama watu wanaojisikia zaidi.

CRISTIANO Ronaldo ni mmoja wa wanasoka maarufu zaidi duniani. Huduma yake bora ndani ya uwanja imemfanya staa huyo kuvuna Pauni 500,000 kwa wiki huko Juventus, huku akiwa anapiga pesa nyingine kupitia udhamini wa kampuni za Nike, Electronic Arts na Herbalife, sambamba na kampuni zake mwenyewe za mavazi ya CR7, viatu na nguo za ndani.
Amecheza Manchester United na Real Madrid kwa mafanikio makubwa kabla ya kwenda kujiunga na Juventus mwaka jana na kuwa mmoja wa mastaa walioshinda ubingwa wa ligi kwenye nchi tatu tofauti, England, Hispania na Italia.
Mashabiki kibao wamekuwa wakimpenda kwa soka lake, lakini mwenye mafanikio hakosi pia wanaomkosoa, na ndio maana Mreno huyo ni moja ya wakali wasiopendwa pia ndani ya uwanja, wakitazamwa kama watu wanaojisikia zaidi.
Lakini, hizi hapa sababu nyingi zinazofanya kwanini Ronaldo hapaswi kuchukiwa kutokana na kile anachokifanya kupitia mafanikio yake kwenye soka, ikiwamo tukio la hivi karibuni kuwatafuta wanawake watatu waliokuwa wakimpa chakula kipindi hicho alipokuwa mdogo akienda kuomba huko kwenye mgahawa wa McDonald’s.

1) Kiatu chake cha dhahabu cha Ulaya
Mwaka 2011, Ronaldo alishinda Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya baada ya kufunga mabao 40 kwenye kikosi cha Real Madrid akiwa chini ya kocha Jose Mourinho. Ronaldo alishinda tuzo hiyo licha ya timu yake kumaliza nafasi ya pili kwenye La Liga na kuishia nusu fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini, badala ya kwenda na tuzo hiyo kuiweka kwenye kabati lake kama kumbukumbu, Ronaldo aliamua kuiuza na pesa alizopata, Pauni 1.2 milioni alizitumia kwa kutoa msaada wa kujenga shule katika eneo lililoathiriwa na vita huko Gaza.

2) Tuzo yake ya Ballon d’Or
Ronaldo alirudia tukio la kuamua kuuza tuzo zake baada ya kufanya hivyo alipotwaa tuzo yake ya Ballon d’Or aliyobeba mwaka 2013 kwenye tukio la uchangishaji wa hisani huko London. Katika tukio hilo, Ronaldo alichagisha pesa kusaidia Make-A-Wish Foundation - inayojihusisha kutoa huduma kwa watoto wenye maradhi mbalimbali ikiwa ya kansa ili kufikia mafanikio yao. Ronaldo alichagia Pauni 530,000 kwenye mradi huo na kuwa mmoja wa wachezaji wenye moto mkubwa wa kujitolea.

3) Balozi wa watoto
Ronaldo ameendelea umaarufu wake aliopata kwenye soka kuwatumia watu. Staa huyo ni balozi wa mashirika makubwa matatu ya umoja wa mataifa inayojihusisha zaidi na watoto kama Save the Children, Unicef na World Vision. Kupitia ubalozi wake kwenye mashirika hayo, Ronaldo amekutana na watoto wengi wenye matatizo kitu ambacho alikwenda kukiweka wazi kwenye hotuba yake wakati anabeba tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2014. Ronaldo amekuwa akipiga vita mambo yote yanayoonekana kuwa na athari kubwa kwa watoto.

4) Bonasi zake za ushindi
Ronaldo amekuwa mtu asiyechoka kujitolea na kwamba amefanya hivyo kwa kutumia mapato yake ya ziada yanayotokana na mafanikio yake ya uwanjani. Mwaka 2013 alipochaguliwa kwenye timu bora ya mwaka ya Ulaya, alipata bonasi ya Euro 100,000 (Pauni 89,000) kutoka Uefa na badala ya kuchukua mkwanja huo akafanyia mambo yake, aliamua kuupeleka Red Cross ukasaidie shughuli mbalimbali za taasisi hiyo. Mwaka uliofuatia, baada ya kushinda ubingwa wa Ulaya, Ronaldo alipewa bonasi ya Pauni 450,000 na Real Madrid na alitoa pesa hiyo yote kwenye mashirika ya Unicef, World Vision na Save the Children.

5) Kuchangia damu
Mwanasoka huyo wa Kireno amekuwa na kampeni ya kupinga uchoraji wa tattoo kwenye mwili ili kuwa na uwezo wa kuchangia damu inapohitajika kufanya hivyo. Ronaldo na ustaa wake wote, hajawahi kuthubutu kujichora tattoo kwenye mwili wake na anafanya hivyo makusudi kwa sababu hataki kuingiza sumu kwenye mwili wake jambo litakalomzuia kuwa mchangiaji wa damu na ute wa mifupa. Staa huyo anafahamu wazi kuweka wino kwenye mwili kuna hatari kubwa ya kuathiri damu kitu ambacho kitamfanya awe na ugumu kwenye kufanya kitu anachokipenda cha kuchangia damu wengine kwa hiari.

6) Msaada wa pesa
Mwaka 2015, Ronaldo alitoa pesa nyingi sana kusaidia waliathirika na tetemeko la ardhi huko Nepal. Janga hilo liliripotiwa kusababisha vifo vya watu 9,000 na kujeruhi 22,000 huku wengi wakikosa mahali pa kuishi. Ronaldo aliripotiwa kuchangia Pauni 5 milioni kwenye msaada wake wa pesa kupitia kwa shirika la Save the Children, licha ya kwamba hakutaka kujieleza wazi kuhusika kwenye kusaidia waliopata matatizo hayo ya tetemeko la ardhi.

7) Asaidia taasisI ya kansa
Mama yake Ronaldo, Dolores Aveiro, aliwahi kusumbuliwa na kansa ya matiti mwaka 2007. Kutokana na hilo, staa huyo alitoa shukrani kwa taasisi iliyomtibu mama yake huko ureno, kwa kuwapa Pauni 120,000 kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za uendeshaji wa taasisi hiyo ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi na kutoa tiba bora kwa wanaohitaji kufanya hivyo. Ronaldo hakutaka jambo hilo lipite tu na kuamua kutoa kile alichokuwa nacho ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kupambana na maradhi ya kansa.

8) Mwaliko kwa yatima
Katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, shabiki wa Real Madrid, Haidar alikuwa yatima baada ya wazazi wake wote wawili kuuawa kwenye bomu la kujitoa mhanga. Mwandishi mmoja wa habari alimfikishia Ronaldo taarifa za kuhusu kijana huyo kiasi cha kumfanya Ronaldo aguswe na kumwalika kijana huyo kwenda kutembelea klabuni Real Madrid kama sehemu ya kumfariji. Kijana huyo ni shabiki mkubwa wa Ronaldo, hivyo wawili hao walipokutana, mtoto Haidar hakuwa na jambo jingine zaidi ya kuangua kilio tu kwa kukutana na shujaa wake.

9) Kumsaidia mtoto mgonjwa
Ronaldo aliguswa na stori ya mtoto Nuhuzet Guillen, aliyekuwa na umri wa miaka tisa kuhusu kuumwa saratani mwaka 2009. Baada ya kusikia taarifa hizo, Ronaldo aliamua kumtuma dereva wake kwenda kumchukua mtoto huyo na familia yake na kuwapeleka kwenye timu ya Real Madrid mahali walikokuwa wamefikia. Baada ya hapo, Ronaldo alimwalika mtoto Nuhuzet, kwenda kutazama mechi uwanjani Bernabeu, tena akikaa kwenye eneo la watu maarufu na kumpatia jezi aliyochezea mechi hiyo. Ronaldo alisema hakuwa na kitu kingine cha ziada ambacho kingemfaa kumfanyia mtoto huyo zaidi ya kumwonyesha yeye ni muhimu na anajaliwa.

10) Kuvamiwa uwanjani
Ronaldo ni moja ya wachezaji ambao mara nyingi mashabiki wamekuwa wakivamia uwanjani kwenda kumsogelea. Lakini, staa huyo mara zote amekuwa akionyesha upendo kwa mashabiki hao bila ya kujali kwamba wanaweza kuhatarisha maisha yake. Kuna wakati, hata staa huyo aliamua kupiga nao picha za selfie mashabiki walioingia uwanjani wakati mechi ikiwa inaendelea. Kuna tukio moja lilimwonyesha Ronaldo akizungumza na shabiki aliyeingia uwanjani na kuwafanya walinzi wa uwanjani kuwa na subira kuliko kumtoa shabiki huyo mbiombio uwanjani.

11) Kumsaidia mtoto mwingine
Mwaka 2014, mama wa mtoto mwingine, aliyekuwa na umri wa miezi 10, Erik Ortiz Cruz, alimwomba Ronaldo kumpatia jezi mtoto huyo aliyekuwa mgonjwa wa akili. Lakini, baada ya kusikia hadithi ya mtoto, Ronaldo aliguswa sana na badala ya kutoa jezi tu, bali alilipa Pauni 55,000 ili mtoto huyo afanyiwe upasuaji wa ubongo kumaliza tatizo lake kwa sabbu ndicho kitu kilichokuwa kikisumbua. Kwa bahati nzuri, mtoto Erik Ortiz Cruz alipona matatizo yake baada ya upasuaji huo.

12) Kumvunja mtoto mkono
Katika mechi moja ya kujiandaa na msimu dhidi ya Bournemouth, Ronaldo alipiga shuti jukwaani kwenye uwanja wa Vitality na bahati mbaya shuti hilo liliishia kwenda kumvunja mkono mtoto wa miaka 11, Charlie Silverwood. Rais wa Real Madrid, timu aliyokuwa akiichezea Ronaldo wakati huo, alimwalika mtoto Charlie na Ronaldo alimpatia jezi yake katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tukio ambalo lilimfanya kijana huyo kusahau machungu ya kuvunjika mkono, lakini kubwa akifurahia kile kilichofanyika kwenye kuonyesha thamani yake.

13) Rafiki wa kweli
Wakala Jorge Mendes amesema Ronaldo kuwa ni rafiki wa kweli wakati alipofunga ndoa na mrembo Sandra mwaka 2015. Katika tukio hilo, Ronaldo aliamua kumpa wakala huyo zawadi matata kabisa, akimnunulia kisiwa kimoja huko Ugiriki. Kisiwa hicho kilimgharimu Ronaldo kiasi cha Pauni 40 milioni, lakini alitoa mkwanja huo mrefu kwa ajili ya kumpa rafiki yake, ambaye pia ndiye wakala wake zawadi itakayodumu kwenye maisha yake yote bila ya kusahau.

14) Awapa zawadi wachezaji wenzake
Baada ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, kila mchezaji wa Real Madrid alipata bonasi ya kufanya hivyo, lakini Ronaldo aliamua kuwaongezea wachezaji wake kwa kuwapa zawadi ya saa za kifahari aina ya Bulgari. Ronaldo alitoa saa hizo kwa kikosi kizima Real Madrid na kila saa moja ilikuwa ya thamani ya Pauni 5,000.