Kumekucha
MWANDISHI WETU KUNA mambo mawili yatakuwapo leo Jumamosi. Kwanza, Ligi Kuu Bara itaanza katika viwanja mbalimbali, na pili, mashushushu wa Recreativo Libolo ya Angola watakuwapo jukwaani katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakiipiga chabo Simba. Kubwa zaidi ni kuwa Kocha Mfaransa wa Simba, Patrick Liewig leo Jumamosi ataanza kuonyesha ufundi wake wakati timu hiyo itakapocheza mechi yake ya kwanza ya mzunguko wa pili dhidi ya African Lyon, lakini anahitaji kushinda mechi mbili mfululizo na aiombee Yanga ipoteze michezo kama hiyo ili kuifikia kilele tayari kwa mkao wa ubingwa. Mfaransa huyo ameichukua Simba hivi karibuni baada ya kupigwa chini kwa Mserbia Milovan Cirkovic, ambaye tangu aondoke hawezi kumaliza siku mbili kabla hajaandika kitu au kuweka picha yoyote ya Simba kwenye ukurasa wake wa facebook. Simba yenye pointi 23 ikishinda mechi hizo mbili mfululizo itakuwa na pointi 29 kama za Yanga ambayo leo Jumamosi itakuwa jukwaani kama mashushushu wa Recreativo Libolo ya Angola itakayocheza na Simba mwezi ujao katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga itaanza kazi kesho Jumapili na Prisons Uwanja wa Taifa. Patrick ametangaza kwamba timu yake iko safi na atatumia uzoefu wake kufanya kazi ambayo itaipa Simba mafanikio kwenye ligi ya ndani na michuano ya kimataifa na kwamba amejifunza mengi kwenye kambi ya Oman na anaijua Simba kiundani. Kocha wa Yanga, Ernest Brandts ameweka wazi kwamba anataka kushinda mechi nane mfululizo za kwanza halafu asome uelekeo wa wapinzani wake wa karibu ambao ni Simba na Azam. Simba ilikuwa imepiga kambi ya wiki mbili nchini Oman. Yanga ilikuwa Antalya, Uturuki huku Azam ikitembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Kenya. Timu pekee inayochukia kushinda mechi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara; Polisi Morogoro itacheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri huku wenyeji wa Tanga Coastal Union na Mgambo wakicheza mkoani kwao. Timu zilizofanya usajili wa bei chee zaidi za Ruvu Shooting na JKT Ruvu ambao ni watoto wa bosi mmoja watacheza Mlandizi huku JKT Oljoro ya Arusha ikicheza na Toto African, ambayo haina hata uhakika wa mlo wa siku na wachezaji wake hawajawahi kusikia kitu kinaitwa mshahara miezi sita iliyopita. Azam ambayo wachezaji wake wanaishi maisha ya raha zaidi jijini Dar es Salaam kutokana kulipiwa gharama nyingi za maisha na muajiri wao itacheza na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Chamanzi ambao ndio wa kisasa zaidi kumilikiwa na timu binafsi. Ligi Kuu ya Bara itamalizika Mei 18.