Kumbe KMC inapigika bila makocha

Thursday October 21 2021
kmc pic
By Daudi Elibahati

KIPIGO cha juzi kwa KMC dhidi ya Yanga kilikuwa cha pili msimu huu na kuwarudisha hadi mkiani mwa msimamo, lakini usichokijua ni kwamba timu hiyo inacheza mechi zake bila makocha wao, Kocha Mkuu John Simkoko mwenye matatizo ya kifamilia, huku msaidizi wake Habib Kondo anasoma.

Hata hivyo, uongozi wa KMC umesema kutokuwepo kwa makocha hao kwenye mechi dhidi ya Yanga iliyopigwa mjini Songea na kulala 2-0 kunatokana na sababu maalumu na kwamba timu itakuwa chini ya msaidizi mwingine, Hamad Ally hata kwenye mchezo ujao dhidi ya Namungo.

Ofisa habari wa KMC, Christina Mwagala alisema kutokuwepo kwa Simkoko ni kutokana na sababu za kifamilia, kwani tangu msimu umeanza hakuwa sehemu ya benchi la ufundi.

“Anashughulikia matatizo ya kifamilia yanayomkabili, hivyo baada ya muda sio mrefu atarejea kuendelea na programu za timu,” alisema Christina aliyeongeza kuwa kipindi hiki timu itakuwa chini ya Hamad.

“Tuna makocha wasaidizi wawili - Kondo na Hamad, hivyo kwa sasa Hamad ndiye ataongoza timu hadi kwenye mchezo ujao dhidi ya Namungo FC,” alisema huku Kondo akifichua kukosekana kwake kwenye kikosi hicho kwa wiki mbili baada ya kuanza mafunzo ya ukocha.

“Niko Morogoro naendelea na kozi ya ukocha leseni B ya Caf. Ni matumaini yangu mchezo wetu ujao na Kagera Sugar nitakuwa sehemu ya benchi la ufundi,” alisema nyota huyo wa zamani wa Reli Morogoro.

Advertisement

Bila uwepo wa makocha Simkoko na Kondo, KMC ilianza kwa kipigo cha mabao 2-0 na Polisi Tanzania kisha kutoka suluhu na Coastal Union kabla ya juzi kufungwa 2-0 na Yanga na kushika mkia ikiwa kati ya timu tatu ambazo hazijafunga bao lolote hadi sasa kwenye mashindano hayo.

Advertisement