Komba amkuna mwamuzi mkongwe

MWAMUZI wa zamani wa soka nchini, Isihaka Shirikisho amesema anavutiwa na jinsi mwamuzi wa sasa Frank Komba anavyojituma na kuifanya kazi yake kwa ufanisi akiwataka waamuzi chipukizi kuiga mfano huo ili wafike mbali kwenye fani hiyo.

Komba ambaye ni wakili na Polisi amekuwa kwenye ubora ndani na hata mechi za kimataifa kutokana na uwezo na umakini alionao anapokuwa katika majukumu yanayomfanya kuzidi kuaminiwa.

Mkongwe huyo aliliambia Mwanaspoti, Tanzania ina waamuzi wengi wenye uwezo mkubwa ila anamtolea mfano Komba kutokana na namna alivyokuwa akipenda kujifunza vitu vingi kutoka kwa waliomtangulia.

“Unajua licha ya elimu kubwa aliyokuwa nayo Komba, huwa hajali huyu ana elimu au la, hadharau mtu na amekuwa akimheshimu kila mmoja. Kwa kweli ana heshima sana yule kijana namuona mbali zaidi ya hapo alipokuwa sasa, mafanikio aliyonayo ni kutokana na juhudi zake hajawai kuchoka,” alisema Shirikisho.

Shirikisho aliwataka waamuzi wengine kujitahidi kuzifuata Sheria 17 ili kuepuka sintofahamu kutoka kwa mashabiki wanaosema waamuzi hawafai.