Kocha Singida FG atimka kambini
Maswali na hoja lukuki zimeibuka kwenye mitandao ya kijamii zikidai kocha wa timu ya Singida Fountain Gate, Ernst Middendorp ameondoka kambini lakini uongozi wa timu hiyo kupitia Ofisa habari wake, Hussein Masanza ametolea ufafanuzi akisema kocha ameenda kutatua changamoto zake binafsi na kutaka wamuombee amalize mapema.
“Ni kweli kocha wetu Ernst ameondoka kwa dharura lakini sio kwa sababu zinazotajwa, kocha na yeye ni binadamu kuna changamoto zake binafsi anapitia na ameenda kuzitatua.
Ningeshauri tumpe nafasi na tumuombee azimalize mapema ili arejee kwenye majukumu yake. Mwarabu bado hatujamalizana nae,” amesema Masanza.
Kocha Middendorp amejiunga na timu Singida akichukua mikoba ya Hans van der Pluijm raia wa kwa Uholanzi na kupewa mkataba wa mwaka mmoja.
Middendorp aliwezesha timu hiyo kutanguliza mguu mmoja makundi Kombe la Shirikisho Afrika baada ya Septemba 17 kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Future ya Misri katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.