Kocha Prisons: Ligi imekuwa ngumu, wachezaji wanatafuta soko

Muktasari:

  • Huo ulikuwa mchezo wa tano kwa Prisons wakicheza bila ushindi ikiwa ni sare nne na kupoteza moja na kubaki nafasi ya tano kwa pointi 30, huku Kagera Sugar akibaki nafasi ya saba kwa alama 26

Mbeya. 'Ligi ni ngumu, wachezaji wanatafuta soko'. Ni kauli ya Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons,  Ahmad Ally akieleza msoto wa mechi tano mfululizo bila ushindi baada ya suluhu dhidi ya Kagera Sugar, Jumatatu.

Prisons ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa imelazimishwa suluhu dhidi ya wapinzani hao ikiwa ni mechi ya tano bila kuonja ushindi tangu iliposhinda dhidi ya Simba mabao 2-1, Machi 6.

Baada ya kuona kikosi chake kinashindwa kupata ushindi, kocho huyo wa Prisons alisema ligi inavyoelekea ukingoni imezidi kuwa ngumu kwa sababu kila mchezaji anacheza kwa nguvu zote akijaribu kutafuta soko.

Hata hivyo, mambo si mabaya sana kwa Prisons ikiendelea kubaki kwenye nafasi tano za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara licha ya kutoka patupu bila ya kuonja ushindi katika mechi tano zilizopita.

"Ligi inaelekea ukingoni wachezaji wanajituma na kufanya mechi zote kuwa ngumu, kila mmoja anatafuta soko kwa ajili ya msimu ujao hata hivyo vijana wangu wamefanya vizuri," alisema kocha Ally

"Ukiangalia mechi tulizokutana nazo, timu zote tunalingana uwezo ndio maana sare zinakuwa nyingi, wala haikutumika nguvu nyingi kwa Simba kwa sababu kila mchezo na mbinu zake" amesema Ally.

Kocha huyo ameongeza kuwa leo haikuwa bahati yao kwani walipata nafasi za kufunga, lakini hawakuzitumia na kwamba wapinzani walikuwa wa kujilinda muda wote.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Kagera Sugar,  Fredi Felix 'Minziro' amesema licha hesabu zao kutafuta ushindi kama walivyofanya mechi iliyopita dhidi ya Tabora United, lakini Prisons walikuwa imara.

Amesema wamepata nafasi kadhaa lakini hawakuwa makini kuzitumia na kwamba wanaenda kusahihisha makosa kabla ya mchezo ujao wa ligi hiyo.