Kocha Ndanda fulu kicheko
Muktasari:
Nawanda alisema wamefanya usajili mzuri mchanganyiko wakiwemo wazoezi na chipukizi huku akiamini timu yake itakuwa tishio mzimu ujao.
KOCHA Msaidizi wa Ndanda, Shaweji Nawanda amesema amefurahishwa na ushindani unaoonyeshwa na wachezaji wake kikosini katika michezo ya kirafiki waliyocheza kujiandaa na Ligi Kuu Bara, akiamini utawabeba ligi ikianza wiki ijayo.
Nawanda amesema katika miaka ambayo wameanza vizuri maandalizi kwa ajili ya Ligi kuu basi mwaka huu ni zaidi kuliko yote.
Ndanda ilifanya ziara maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya za Masasi na Namtumbo na kucheza mechi za kirafiki ikiwa ni maandalizi yao kujiandaa na ligi itakayoanza mwishoni mwa mwezi huu.
Nawanda alisema wamefanya usajili mzuri mchanganyiko wakiwemo wazoezi na chipukizi huku akiamini timu yake itakuwa tishio mzimu ujao.
"Tumeanza maandalizi ya kishindo kwa kucheza baadhi ya mechi za kirafiki na lengo ni kujiweka sawa kwa ajili ya ligi.
"Najivunia kikosi changu kwani tumefanya usajili mzuri ambao naamini utakuwa na manufaa kwetu kwa kuiwezesha timu kufanya vizuri," alisema Nawanda.
Wakati huo huo timu hiyo imemtangaza Kocha Malale Hamsini kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho akisaini mkataba wa mwaka mmoja.
Malale anachukua nafasi ya Khalid Adam aliyekuwa na timu hiyo msimu uliopita lakini sasa amerejea kuifundisha timu ya Mwadui ya Shinyanga.