Kocha Mtunisia atua Yanga, aanza hivi

Tuesday April 20 2021
mpya pic
By Mwandishi Wetu

KAMA Mwanaspoti lilivyokufichulia mara ya kwanza jana ni kwamba Mtunisia Nasreddine Nabi ndiye kocha mpya wa Yanga na atatua nchini leo saa 7:30 mchana.

Awali, Yanga ilishamalizana na Kocha Mfaransa, Sebastian Migne, lakini akawa na masharti madogomadogo mengi kila mara jambo ambalo liliwashtua mabosi na kuachana naye juzi kabla hajatua asije kuwasumbua mbele ya safari.

Nabi ambaye ana uraia wa Tunisia na Ubelgiji, alikuwa kwenye benchi la Al Merrikh kwa muda mfupi walipotoka suluhu na Simba jijini Khartoum na ile ya Dar es Salaam walipokula mabao 4-0 alishaachana nao. Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba usiku wa leo atakuwa Kwa Mkapa kuicheki timu hiyo ikikiwasha na Gwambina na kesho atakwenda kambini. Mechi yake ya kwanza benchi itakuwa Jumapili dhidi ya Azam.

Habari za ndani ya Yanga zinasema Nabi ambaye ana uzoefu na soka la Afrika akibeba ubingwa mara kadhaa nchini DR Congo na Sudan, amepewa mambo manne ya kuanza nayo Jangwani.

Mmoja wa vigogo ndani ya Yanga alidokeza jana kwamba wamemuambia Nabi mambo manne; aondoe makundi ndani ya timu, arudishe nidhamu ya ndani na nje ya uwanja, arudishe ari ya upambanaji na soka lenye mvuto na mwisho afikirie muundo wa kikosi kipya cha michuano ya Afrika.

Mabosi wa Yanga wamemwambia pamoja na hali iliyopo ila wanataka apambane kupata matokeo katika mechi zote zilizosalia kwani bado wapo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi na FA.“Tuna nafasi ya kupata kombe moja au mawili ligi haijaisha, kwa hiyo hilo la kwanza lakini katika hili atatakiwa kubadilisha uwezo wa timu kucheza, kwa sasa timu inacheza kawaida sana, tunashinda kwa presha sana,” alidokeza mmoja wa mabosi wa Yanga akisisitiza wana imani na uzoefu wake.

Advertisement


REKODI ZAKE

Nabi ana leseni ya Uefa na mwaka 2012 alibeba Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na AC Leopards ya DR Congo.

Aliwahi kuwa kocha mkuu wa Ismailia ya Misri, Al Hilal na Al Ahli Benghazi za Sudan na DC Motema Pembe na AC Leopards za DR Congo. Amebeba ubingwa mara mbili nchini DRC, amecheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Shirikisho na kubeba ubingwa wa Shirikisho.

Advertisement