Kocha mpya Simba SC Mholanzi, Mnigeria wapeta

Muktasari:
Mwanaspoti limefanikiwa kuyanasa majina ya makocha hao ambao ni Zlatko Krmpotic (raia wa Serbia), Paul Aigbonun (Nigeria), Frank Nuttal (Scotland), Nelson Eduardo Silva Santos (Mreno), Ivan Minnaert (Ubelgiji), Abdelali Gsaib (Morocco), Cavin Johnson (Afrika Kusini) na Hendrik Pieter de Jong raia wa Uholanzi.
BILIONEA na mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji (MO) juzi ameweka bayana mchakato wa kumpata mrithi wa Patrick Aussems, uko kwenye hatua za mwisho kukamilika.
Hata hivyo, Mwanaspoti ambalo limekuwa likifuatilia kwa karibu mchakato huo, limepenyezewa tayari majina ya makocha wanane kati ya 52 walioomba kazi hiyo, yameshapatikana baada ya kazi ya kuyafanyia mchujo kukamilika juzi.
Imeelezwa kazi ya kuchambua sifa za makocha hao ilifanyika kwa umakini mkubwa chini ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingiza na mchujo wa mwisho ulitarajiwa kukamilika muda wowote kuanza jana kisha kubaki watatu ambao watakwenda kufanyiwa usaili na Kamati ya Salum Madadi. Kamati hiyo ndio iliyomfanyia usaili Aussems wakati akipewa kibarua cha kuinoa Simba miaka miwili iliyopita. Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga, Mkufunzi wa Makocha wa TFF, Sunday Kayuni na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo.
Kazi ya Kamati hiyo ambayo tayari imeanisha vigezo na sifa ambazo anatakiwa kuwa nazo mwombaji, itapelekewa orodha ya wasifu wa makocha hao watatu bila kuwepo kwa majina ili kuondoa mgongano wowote wa kimasilahi kisha wakikamilisha kazi watayarejesha kwa mabosi yakiwa pamoja na mapendekezo ya mtu sahihi.
Mwanaspoti limefanikiwa kuyanasa majina ya makocha hao ambao ni Zlatko Krmpotic (raia wa Serbia), Paul Aigbonun (Nigeria), Frank Nuttal (Scotland), Nelson Eduardo Silva Santos (Mreno), Ivan Minnaert (Ubelgiji), Abdelali Gsaib (Morocco), Cavin Johnson (Afrika Kusini) na Hendrik Pieter de Jong raia wa Uholanzi.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua licha ya mchakato huo utapitia kwa Kamati ya Madadi, lakini Simba inapendelea zaidi kumpata kocha ambaye ataifanya timu hiyo kucheza soka la kushambulia na kumiliki mpira muda wote.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limepenyezewa na kigogo mmoja wa Simba, wanataka kubadilisha kabisa mfumo wa uchezaji kutoka wa sasa kwenda total football ambao asili yake ni Uholanzi.
“Tunataka kutengeneza timu sio ya kushinda uwanjani tu bali mashabiki wafurahia kuona timu ikicheza. Burudani ya soka wachezaji wapige pasi kuanzia nyuma hadi langoni mwa adui na kufunga pale wanapotaka…huu mpira wa butua butua hatutaki na ndio sababu tunataka kuleta total football Tanzania,” alisema kiongozi huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Aliongeza Simba ambayo imejipambanua kuwa klabu inayojiendesha na kupanga mambo yake kisasa, inataka kutengeneza staili ya soka la kushambulia huku ikimiliki mpira muda wote wa mchezo.
“Tumeona CV za kocha wengi lakini naamini kwa sifa na vigezo vya hawa waliopita kwenye mchujo basi tutapata bonge la kocha …ngoja tuache kwanza kamati iliyopewa kazi ikamilishe majukumu yake.”
Kwa upande wake, Mazingisa alipoulizwa kuhusu mchakato huo alisema, wapo katika hatua za mwisho kukamilisha na anaamini katika kocha mwenye kiu ya mafanikio na kutimiza malengo.
Alisema kwake sio muumini mzuri sana wa wasifu wa makocha bali kocha mwenye kusimamia vyema majukumu yake na kuipa timu mafanikio ndio bora zaidi.
“Ni suala la muda mfupi uliobaki na siku si nyingi tutatangaza kocha mpya, ambaye atakuja kuifundisha Simba. Ndio tunamalizia mchakato, lakini kuhusu hao makocha wanane walitajwa kuingia katika orodha ya mwisho.”
Mwanaspoti liliwasiliana na Mirambo ili kufahamu mchakato huo ulipofikia na alikiri kuwa mmoja wa wanakamati.
Hata hivyo, Mirambo amesema bado majina hayajawafikia kwa ajili ya kufanya mchakato huo, lakini kwa utaratibu ulivyo hukabidhiwa nyaraka ikiwemo wasifu wa waombaji siku ya usaili.
“Ni kweli kuna huo mchakato wa kuwafanyia usaili makocha walioomba kazi Simba, lakini bado hawajapewa taarifa kuhusu siku rasmi ya kuifanya kazi hiyo. Kama ilivyokuwa kwa Aussems… sisi kazi yetu ni kupitia wasifu na kuangalia vigezo vyao kama vinaendana na matakwa ya Simba, kisha tunatoa mapendekezo yetu kwa hatua zaidi,” alisema.