Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Morocco asifu nidhamu ya kimbinu

Muktasari:

  • Bao lililofungwa dakika ya 89 na beki wa kulia Shomary Kapombe lilitosha kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa pili mfululizo kwenye mashindano hayo na kufikisha pointi sita ambazo zinaifanya timu hiyo kuongoza msimamo wa kundi B.

KATIKA mechi iliyojaa tahadhari na vita ya kimbinu, Taifa Stars  imeendelea kung’ara kwenye Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania, Jumatano usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Bao lililofungwa dakika ya 89 na beki wa kulia Shomary Kapombe lilitosha kwa Taifa Stars kuibuka na ushindi wa pili mfululizo kwenye mashindano hayo na kufikisha pointi sita ambazo zinaifanya timu hiyo kuongoza msimamo wa kundi B.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’, alielezea kufurahishwa kwake na nidhamu ya kimbinu iliyoonyeshwa na vijana wake, akisema mechi hiyo ilikuwa ni vita ya mbinu zaidi ya uwezo binafsi wa wachezaji.

“Tulijua mchezo huu hautakuwa rahisi. Mauritania walicheza kwa kujilinda na kutupa presha kwa mipira mirefu. Lakini tulijipanga, tukafanya mabadiliko muhimu na tukapata matokeo,” alisema Morocco.

Kocha huyo aliwashukuru mashabiki wa Tanzania kwa sapoti ya hali ya juu na kusisitiza kuwa nguvu hiyo ya jukwaani ilichangia kuongeza morali kwa wachezaji wake.

“Tulianza mchezo kwa shida, lakini tulikuwa tumefanya maandalizi ya kutosha. Mabadiliko ya wachezaji tuliyofanya yalibadilisha mchezo. Walifuata maelekezo na tukafanikiwa kushinda.”


HESABU ZA MOROCCO

Kocha Morocco alikiri kuwa pamoja na ushindi huo, yapo maeneo ambayo wanahitaji kuyaboresha kabla ya mechi inayofuata Jumamosi dhidi ya  Madagascar, hasa katika eneo la umaliziaji.

“Tunaenda kufanya kazi zaidi mazoezini. Tunahitaji kuboresha ufanisi wetu mbele ya lango. Si rahisi kufunga bao ukiwa unapambana na timu inayotumia wachezaji sita au saba kujilinda. Tulihimili kipindi cha kwanza, na kipindi cha pili tukabadili kasi,” alisema.


LOPEZ: HATUKUSTAHILI KUPOTEZA

Kocha wa Mauritania, Aritz Lopez Garai kutoka Hispania, alionyesha masikitiko yake kwa matokeo hayo, ingawa alisifu juhudi za wachezaji wake na kusema hawakustahili kupoteza.

“Tulicheza vizuri, tulidhibiti mchezo, lakini mpira una tabia ya ajabu. Unaweza kutawala, ukacheza vizuri lakini ukapoteza kwa kosa moja. Tanzania walitumia nafasi moja waliyopata na wakaamua matokeo,” alisema.

Lopez Garai aliongeza kuwa walijaribu kuwazuia Tanzania kwa kujilinda kwa pamoja na kuziba mianya, lakini makosa madogo yalisababisha wapinzani wao kupata bao.


MSIKIE MUDATHIR

KIUNGO wa kati wa Taifa Stars, Mudathir Yahya, amefichua kuwa mshikamano wa kikosi na kutekeleza maelekezo ya benchi la ufundi kwa umakini ndiyo siri ya ushindi wa Tanzania dhidi ya Mauritania, kwenye mechi ya pili ya hatua ya makundi ya michuano ya CHAN 2024 iliyochezwa Jumatano jijini Dar es Salaam.

Mudathir, ambaye ni mmoja wa wachezaji waliocheza kizuri katika mechi hiyo huku akiteuliwa Nyota wa Mchezo, alisema maandalizi ya awali yalikuwa na nafasi kubwa katika matokeo hayo.

“Tumeshinda kwa sababu tulifuata kila tulichoelekezwa na benchi la ufundi. Tulijituma kama timu, tulicheza kwa umoja, na kila mchezaji alijua majukumu yake. Hiyo ndiyo siri kubwa ya ushindi wetu,” alisema Mudathir.

Mudathir, ambaye ni mzoefu kwenye mashindano ya kimataifa, aliongeza kuwa ushindi huo si wa kubeza kwani Mauritania ni timu yenye wachezaji wenye kasi na nguvu. Alisisitiza kuwa Taifa Stars ilihitaji kuwa makini kila dakika.

“Mauritania si timu rahisi, walitupa changamoto kubwa. Lakini tulijipanga vizuri na tulikuwa tayari kwa aina yoyote ya mchezo.”

Katika mechi hiyo, safu ya kiungo ya Tanzania ilifanya kazi kubwa ya kuzuia mashambulizi ya wapinzani huku pia ikipika mashambulizi, jambo lililosaidia Taifa Stars kujiamini na kutawala hasa mwishoni mwa kipindi cha pili.