Kocha Mamelodi kujichimbia ili kuitazama Yanga

BAADA ya kuwafahamu wapinzani wao, kocha wa Mamelodi Sundowns,  Rhulani Mokwena amesema anakwenda kujichimbia kuitazama zaidi Yanga kiufundi wakati wa mapumziko ya kalenda ya mechi za kimataifa.

Hivi karibuni timu za mataifa mbalimbali zitakuwa na michezo ya kirafiki na mashindano ambayo ya kimataifa, kipindi ambacho ligi zote duniani husimama kupisha mechi hizo.

Mokwena amesema binafsi amekuwa akizitazama mechi za timu zote ambazo zilikuwa na uwezekano wa kukutana nazo, lakini anataka kurudia tena ili kuwatazama kwa umakini zaidi Yanga.

Kocha huyu amesema anaiheshimu timu hiyo kwa sababu  ina muunganiko na uongozi mzuri na kocha Miguel Gamondi ni mmoja kati ya makocha bora na ameshawahi kuifundisha timu hiyo (Mamelodi).

"Nitarudia tena kuwatazama kwa umakini zaidi. Niliwahi kutazama mechi zao, lakini sikuwa nimejikita kwenye kuzichambua zaidi, hivyo nitakwenda kuwatazama tena na jambo zuri nitakuwa na muda mwingi kwa sababu tunakwenda kwenye mapumziko ya kalenda ya kimataifa ya Fifa," amesema.

Mokwena amesema hayo wakati anafanya mahojiano na waandishi wa habari baada ya mchezo wa Ligi Kuu Afrika Kusini dhidi ya Supersport United uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mamelodi ni moja ya timu tishio kwa sasa kwenye michuano mbalimbali barani Afrika ikiwa imeanza mwaka vizuri kwa kuchukua Kombe la African Football League baada ya kushinda fainali dhidi ya Wydad Casablanca kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.

Pia kwa sasa inaongoza katika Ligi Kuu Afrika Kusini ikiwa nafasi ya kwanza na pointi 46 baada ya kucheza mechi 18 na ina viporo vya mechi mbili.

Katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilimaliza kinara wa kundi A ikivuna alama 13 baada ya kushinda mechi nne, sare moja na kufungwa moja.

Mchezo wa mkondo wa kwanza baina ya Yanga na Mamelodi unatarajiwa kupigwa kati ya Machi 20 na 30, huku ule wa marudiano ukipigwa kati ya Aprili 5 na 6.