KMC, Mtibwa hakuna mbabe

Monday June 21 2021
mtibwa pic
By Mwandishi Wetu

Ligi kuu Tanzania Bara imeendelea leo kwa timu ya KMC kukaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Mtibwa ndio walitangulia kupata bao la uongozi dakika ya 55 kupitia kwa mshambuliaji mkongwe, Kelvin Sabato kabla ya KMC kusawazisha bao hilo dakika ya 81 kupitia kwa Cliff Buyoya, baada ya makosa ya kiungo wa Mtibwa, Baraka Majogoro kurudisha mpira langoni mwao wakati akijaribu kuokoa mashambulizi ya KMC.

Hata hivyo sare hiyo ya ugenini kwa Mtibwa watalazimika kumlaumu mfungaji wa bao lao Sabato kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga kabla ya kufunga bao lake ambazo zingeweza kuipa faida timu yake.

Katika mchezo huo uliokuwa wa vute ni kuvute ulishuhudia kila timu ikikosa umakini katika lango la mwenzake la kumalizia  nafasi ambazo imezipata.

Matokeo hayo yanaifanya KMC kuendelea kusalia nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi kuu Tanzania Bara kwa kufikisha pointi 42 katika michezo 31 huku ikisaliwa na michezo mitatu dhidi ya Simba, JKT Tanzania na Ihefu.

 Mtibwa Sugar nao  inaendelea kushika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 38 katika michezo 32 ikisaliwa na michezo miwili dhidi ya Dodoma Jiji na JKT Tanzania.

Advertisement


IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI

Advertisement