Kizungumkuti JKT Queens vs Simba Queens, zagawana uwanja

WAKATI wadau na wapenzi wa soka la wanawake wakisubiri mechi ya Ligi Kuu kati ya Simba Queens na JKT Queens saa 10:00 jioni, bado kuna kizungumkuti.

Kizungumkuti kinakuja baada ya JKT kupitia kwa Msemaji wake, Masau Bwire kudai kuwa mechi hiyo imepangwa kuchezwa uwanja wao wa nyumbani, Maj General Isamuhyo uliopo Mbweni na Simba wakidai kuwa wanafuata maelekezo ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuwa mechi inapigwa Azam Complex.

Awali TFF ilitoa ratiba kuwa mchezo huo utapigwa Uwanja wa Isamuhyo lakini jana jioni ilibadilisha ratiba hiyo kupitia ukurasa wa Instagram ikipangwa kuchezwa Azam Complex.

Tetesi zinaeleza kwamba TFF ilitoa barua kwa klabu zote mbili kuhusu mabadiliko ya uwanja ambao wenyeji wa mchezo huo JKT Queens ilidai kuwa haijapata taarifa hizo.

Mwanaspoti lilipomtafuta, Mkurugenzi wa mashindano wa TFF, Baraka Kizuguto alisema kuwa apigiwe simu Ofisa Habari, Clifford Ndimbo ambaye tulimtafuta lakini hakupokea simu.

Kupitia kwenye kundi moja la mtandao wa WhatsApp, Kocha Msaidizi wa Simba Queens Mussa Hassan 'Mgosi' aliandika ujumbe uliosomeka hivi.

"Maswali ya kujiuliza kabla ya propaganda, Uwanja ulifungiwa mpaka utakapomaliza matengenezo, walioufungia uwanja washakuja kukagua matengenezo, mlishafanya marekebisho na kutaka wahusika waje kujiridhisha,

"Walioufungia walitoa tangazo umefungiwa, Je tayari wametoa tangazo, warusha matangazo mubashara wamekagua na vipi kuhusu Email (barua pepe) iliyotumwa Januari 4 na TFF kuhusu kujulisha klabu kuwa mechi ni Chamazi na mlirudisha majibu ya kusema mtatumia uwanja wenu," aliandika Mgosi.

Kwa upande wa JKT, Masau alisema mchezo wao utachezwa uwanja wa nyumbani na tayari timu hiyo ipo uwanjani.

"Ni kweli mkanganyiko upo wa wapi mchezo huo utachezwa lakini sisi bado tunasisitiza kuwa mchezo utachezwa uwanja wetu na tunaamini wapinzani wetu watakuwepo na kama hawatafika sisi tutakuwepo huku kwetu kushuhudia mtanange," alisema Masau.

Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana kwenye Ligi, JKT Queens ilitoka sare ya bao 1-1 kwenye uwanjan wao wa nyumbani na waliporudiana Simba ililala kwa mabao 2-1 nyumbani kwao Mo Simba Arena, Bunju.