Kitasa cha Tabora Utd bado kidogo

BEKI wa kati wa Tabora United Mkongomani, Kelvin Kingu Pemba ameanza kutoa hogo lake la mguu wa kushoto huku ikiwa ni ishara nzuri kwa nyota huyo kukaribia kuanza mazoezi na kikosi cha kwanza baada ya kuvunjika mshipa wake Agosti 31.

Pemba aliyejiunga na timu hiyo msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuachana na klabu ya Mbabane Swallows ya Eswatini, alipata majeraha hayo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Big Stars hivyo kukaa nje miezi miwili.

Akizungumza na Mwanaspoti, daktari wa timu hiyo, Abel Shindika alisema nyota huyo anaanza kurejea taratibu huku akiwa bado kwenye uangalizi wa madaktari ingawa muda sio mrefu ataanza mazoezi binafsi kisha kujumuishwa katika kikosi cha kwanza.

“Awali ilionekana jeraha lake ni la kawaidia lakini tuligundua lina ukubwa wake ndio maana tulimpa zaidi miezi miwili ili apone vizuri, hali yake ya kiafya inazidi kuimarika na muda sio mrefu mashabiki wetu watamuona uwanjani,” alisema.

Kwa upande wa kocha mkuu wa timu hiyo, Goran Kopunovic alisema tangu kuumia kwa nyota huyo kumekuwa hakuna utulivu zaidi katika eneo la kujilinda kwani alishaanza kutengeneza muunganiko mzuri hivyo itakuwa jambo jema akimuona akirejea tena.

“Baada ya kuumia tuliona waliopo wataweza kuziba nafasi yake ila kiukweli matarajio yetu yalienda tofauti kwa sababu ni moja ya wachezaji viongozi uwanjani anayeweza kuunganisha wenzake hivyo kwetu ilikuwa ni pigo kumkosa kwa muda mrefu,” alisema kocha huyo raia wa Serbia ambaye amewahi kuifundisha klabu ya Simba.