Kitambi: Simba hii ‘mchuzi juu’

KOCHA mkuu wa Namungo, Denis Kitambi ametaja siri ya Simba kwamba inatumia zaidi upande wa beki wake Shomari Kapombe katika kupeleka mashambulizi kwa njia ya krosi kwa kutumia neno la ‘mchuzi juu’.

Baada ya mchezo kumalizika, Kitambi alifanya mahojiano na Azam TV na amesema kwamba wapinzani wake aliwasoma na kugundua wanatumia njia hiyo kupeleka mashambulizi.

"Simba inatumia sana upande wa Kapombe kupeleka mashambulizi, anapiga krosi na kwa sisi watoto wa kiswahili tunasema ni njia ya mchuzi juu," amesema Kitambi.

Kitambi amesema aliwasoma wapinzani wake vizuri na kugundua kwamba wana ubora mwingine katika dakika 30 za mwisho kila mchezo na kufunga mabao tisa wakati huo timu hiyo kabla ya mchezo wa jana ilikuwa imefunga mabao 17 hivyo bao walilofunga lilikuwa ni la 18 na la 10 kufunga kwenye dakika 30 za mwisho (kipindi cha pili).

"Ndio maana nilifanya baadhi ya mabadiliko kwenye kipindi cha pili kuhakikisha tunapata matokeo, tulitengeneza nafasi nyingi katika mchezo huu;

"Tulistahili ushindi na sio sare kwa sababu zipo nafasi mbili ambayo moja iligonga mwamba na nyingine haikutumiki vizuri."

Kaimu kocha wa Simba, Daniel Cadena amesema wachezaji wake wamefanikiwa kutawala mechi lakini hawakuwa na bahati ya kupata mabao.

Matokeo hayo yameifanya Simba kuendelea kusalia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 19.