Kipigo cha refa chaiamsha TFF

Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeonya kuwa litatoa adhabu kali kwa mdau au mchezaji wa soka atakayethubutu kufanya tukio la kumpiga mwamuzi kama lililotokea Uturuki juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Uturuki baina ya MKE Ankaragucu na Caykur Rizespor ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Katika tukio hilo lililoibua mjadala mkubwa duniani, Rais wa Klabu ya MKE Ankaragucu, Faruk Koca alimpiga ngumi mwamuzi Halil Umut Meler kwa kile kilichoonekana ni kutoridhishwa na uchezeshaji wa refa huyo.

Tukio hilo lilisababisha kupasuka kwa sakiti ya jicho la Meler ambaye hadi sasa amelazwa akipatiwa matibabu katika moja ya hospitali nchini humo.

Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi ya TFF, Nassoro Hamduni alisema jana kuwa kamati yake inalaani vikali kitendo hicho na haitasita kumshughulikia yeyote atakayefanya au kujaribu kujihusisha na kitendo cha kupiga waamuzi katika shindano lolote la soka nchini.

“Hili ni jambo la ovyo. Tunalilaani na limetusikitisha sana. Inaonekana huyo aliyefanya kitendo cha kupiga mwamuzi alikuwa na chuki zake nyingine binafsi zaidi ya sababu zitokanazo na soka. Sio jambo jema chuki za mtaani kupelekwa uwanjani. Tunaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Uturuki, FIFA (Shirikikisho la Mpira wa Miguu Duniani) na UEFA (Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya).

“Na hili sio Uturuki tu, hata hapa haliwezi kuvumiliwa hata hapa kwetu na atakayejaribu kufanya hivyo ataadhibiwa vikali kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uendeshaji wa mpira wa miguu,” alisema Hamduni.

Kiongozi huyo aliwakumbusha pia waamuzi kuchezesha vyema ili kutotengeneza mazingira ya kushawishi vurugu kama hiyo iliyotokea Uturuki.

“Kamati ya waamuzi inaendelea kuwasisitiza waamuzi kuwa makini na kusimamia vyema sheria 17 za mpira wa miguu. Klabu zinatumia gharama kubwa kujiandaa hivyo mwamuzi anapokuwa makini anaepusha matukio kama hayo. Hapa matukio kama hayo hayapo lakini huwezi kujua nini ambacho mwanadamu anakiwaza,” alisema Hamduni.

Refa mstaafu, Athumani Kazi alisema tukio hilo lililotokea Uturuki ni aibu na familia ya soka inapaswa kuhakikisha halitokei Tanzania kwa sasa wala siku za usoni.

“Mpira una sheria zake 17 pia kuna kanuni zinatakiwa kuzingatiwa na kufuatwa pale mwamuzi au mchezaji anapofanya makosa na wao pia wana kamati zao maalum ambazo zimekuwa zikikaa na kufanya maamuzi.

“Hakuna sehemu inaruhusiwa refa apigwe kutokana na kufanya makosa na ndio maana kuna kamati maalumu zimeandaliwa kushughulikia makosa yanayofanyika baada ya mchezo iwe kwa mchezaji na mchezeshaji baada ya kamati ambayo imepewa jina la masaa 72 wao pia wamekuwa wakiadhibu kwa kufungiwa au kusimamishwa kwa muda hivyo nashauri tuache sheria na kamati zifanye kazi zake.

“Napongeza hatua iliyochukuliwa na rais wa nchi husika italeta nidhamu kwa nchi nyingine ambazo zinajichukulia uamuzi mkononi bila kufuata sheria na kanuni,” alisema Kazi.

Mchambuzi wa soka na nyota wa zamani wa Kikwajuni ya Zanzibar, Ibrahim Masoud ‘Maestro’ alisema tukio hilo ni baya katika mchezo wa soka na linapaswa kuzuiwa lisitokee hapa Tanzania na duniani kote.

“Wapo watu wanaona ni sawasawa kwa sababu wanajaribu kuchukulia yale matatizo ambayo yapo katika ligi ya ndani ya kuhusiana na waamuzi wakiona kama yule refa alistahili alichokipata kwa kulinganisha na yale matukio katika ya hapa nyumbani.

“Lakini tufahamu kwamba FIFA walilazimika kuleta teknolojia sababu ya kufahamu kwamba binadamu ni kawaida kufanya makosa. Inatupa fundisho kwenye pande zote mbili, kwanza kwa mwamuzi ni kuwa makini katika kazi yako. Lakini pili tunapata fundisho hatutakiwi kufanya tukio kama lile na pia tunapata fundisho la kuwa waungwana,” alisema Maestro.

Kutokea kwa tukio hilo, kunakumbushia 2012 ambapo aliyekuwa beki wa Yanga, Stephano Mwasika alimpiga ngumi refa Israel Nkongo katika mechi ya timu yake dhidi ya Azam FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Yanga ilipoteza mabao 3-1.

Tukio hilo lilisababisha Mwasika afungiwe kujihusisha na soka kwa mwaka  mmoja huku wengine walioshiriki Jerry Tegete akifungiwa miezi sita, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mechi sita na Omega Seme na Nurdin Bakari waliofungiwa mechi tatu kila mmoja.

Refa msaidizi Charles Saimon, mwaka 2016 naye alikutana na kadhia kama hiyo baada ya kupigwa jiwe na shabiki ambaye hakujulikana baada ya kutokea kwa vurugu kwenye mechi ya Coastal Union dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Tukio la refa Meler limeonekana kuteka hisia za wengi akiwemo Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan  aliyeagiza hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wote waliohusika nalo.

“Michezo inamaanisha amani na udugu. Michezo haiko sambamba na vurugu. Hatuwezi kuja kuruhusu vurugu zichukue nafasi katika michezo Uturuki,” alisema Erdogan.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino alisema:”Kiujumla haikubaliki na haina nafasi katika mchezo na jamii yetu.  Dakika chache baada ya kutokea tukio la kupigwa, refa Meler alisema, ‘ni kosa langu,” pasipo kuainisha kwa nini hasa yeye ni chanzo cha hilo.