Kipa Simba atajwa Mtibwa, Mashujaa

Muktasari:

  • Mashujaa inashika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara huku Mtibwa ikiburuza mkia kati ya timu 16 zinazoshiriki michuano hiyo.

Timu za Mashujaa FC na Mtibwa Sugar ambazo zinashika nafasi mbili za mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara zinadaiwa kusaka saini ya kipa wa Simba, Hussein Abel katika dirisha dogo la usajili linaloendelea kwa sasa.

Mashujaa inashika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara huku Mtibwa ikiburuza mkia kati ya timu 16 zinazoshiriki michuano hiyo.

Habari ambazo Mwananchi linazo ni kuwa, wakati Mashujaa inafukuzia kumsajili Abel, Mtibwa imeshatuma barua Simba ikimtaka kipa huyo kwa mkopo. Hata hivyo, timu hiyo bado haijajibiwa.

Kwa upande wa Mashujaa, kocha Mohamed Abdallah 'Baresi' ameamua kukisuka upya kikosi chake kilichopanda Ligi Kuu Bara msimu huu na kuanza vyema kikipata matokeo mazuri, lakini ghafla kilianza kupoteza mwelekeo kwa kupoteza michezo na sare zilizokishusha hadi nafasi za chini mwa msimamo wa ligi.

Abel alisajiliwa na Simba msimu huu akitokea KMC na katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara ambazo imecheza ni moja pekee dhidi ya KMC iliyotoka sare ya mabao 2-2 ndio alikaa benchi.

Nyota huyo amekuwa na wakati mgumu ndani ya Simba kutokana na ushindani uliopo kutoka kwa makipa wenzake Ayuob Lakred ambaye sasa anaaminiwa kukaa langoni, Ally Salim huku Aishi Manula  aliyekuwa namba moja yupo nje ya uwanja baada ya kujitonesha jeraha. Hata hivyo, Manula ameitwa kwenye kikosi kinachojiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazotarajia kuanza Januari 13, 2024.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa, huenda kukawa na ugumu kumwachia Abel wakati hakua uhakika juu ya Manula ambaye awali ilielezwa atarejea uwanjani Februari 2024, hivyo ndani ya kikosi kubaki na makipa watatu wa uhakika ukiachana na Ahmed Ferouz ambaye alipandishwa kutoka U20.

Mashujaa inaonyesha kwamba imedhamiria kufanya usajili mkubwa na kwa safu zote, kwani inadaiwa kuwa na mpango wa kuongeza wachezaji 10 wa nafasi tofauti ambao kati yao itawaomba kwa mkopo kutoka timu zingine akiwemo Tariq Seif wa JKT Tanzania na Masoud Abdallah 'Cabaye' wa KMC.

Alipotafutwa kuzungumzia suala la usajili, Baresi alisema: "Nimewapa ripoti mabosi wangu, hivyo natarajia itafanyiwa kazi ili tuwe na kikosi imara zaidi. Nani namhitaji? Basi ni suala la muda utakapofika wa kukamilisha kila kitu."