Kipa Azam avunja ukimya kisa...

Friday November 26 2021
kigonya pic
By Daudi Elibahati

KIPA wa Azam FC Mathias Kigonya amesema kuwa lawama anazopata kutokana na mabao anayofungwa anachukulia kama changamoto kwake ya kufanya vizuri.

Kauli ya kipa huyo inakuja baada ya kufungwa bao la pili na kiungo wa KMC, Hassan Kabunda kwa mpira alioutema eneo la 18 hivyo kusababisha timu hiyo kupoteza kwa mabao 2-1, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Uhuru.

“Hakuna anayependa timu yake ifungwe, huwa inatokea kulingana na mchezo ulivyo, lawama zimekuwa nyingi juu ya mabao hayo lakini nazichukulia kama changamoto kwangu ili ziweze kunifanya bora zaidi ya hapa,” alisema.

Bao hilo sio la kwanza kwa kipa huyo kufungwa kwani alifanya makosa kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC baada ya kuutema mpira kisha beki wa timu hiyo Ali Gabr kufunga bao lililowaondosha kwenye michuano hiyo.

Kwa upande wa winga wa kikosi hicho Iddy Seleman ‘Nado’ alisema kuwa bado ana matumaini na kikosi hicho maana hata msimu uliopita walianza vizuri licha ya kumaliza vibaya.

“Tunayo nafasi ya kukaa kama wachezaji na benchi letu la ufundi kujua tatizo nini kwa sababu tuna kikosi bora ambacho kinaweza kufunga timu yeyote, hivyo ni suala la muda tu kwani kila kitu kitaenda sawa,” alisema Nado.

Advertisement

Katika michezo sita iliyocheza imeshinda michezo miwili dhidi ya (Geita Gold, Namungo) wakapoteza mitatu (Yanga, KMC na Polisi Tanzania) kisha wakatoka sare na Coastal Union hivyo kuwafanya kushika nafasi ya 10, wakiwa na alama saba.

Advertisement