KINDOKI: De Gea wa Yanga aliyetuliza mashabiki mizuka

Muktasari:

Kila wakionyesha nia kwa mchezaji, kabla hajaanza hata harakati za kusaka saini yake, tayari Simba wanavamia na kumbeba fasta tu. Hatua hiyo iliwafanya viongozi wa Yanga kutuliza akili na kuendesha mambo kimyakimya kwa weledi mkubwa, jambo lililiwawezesha kunasa mastaa wa maana.

USAJILI wa Yanga ulianza kwa kusuasua kutokana na ukata, lakini mabosi wake walikuwa wakifahamu ni kitu gani wanafanya.

Kila wakionyesha nia kwa mchezaji, kabla hajaanza hata harakati za kusaka saini yake, tayari Simba wanavamia na kumbeba fasta tu. Hatua hiyo iliwafanya viongozi wa Yanga kutuliza akili na kuendesha mambo kimyakimya kwa weledi mkubwa, jambo lililiwawezesha kunasa mastaa wa maana.

Awali, tatizo kubwa ndani ya Yanga lilikuwa ni kipa na mashabiki wa Jangwani hawakuwa wakimkubali kipa wao namba moja, Youthe Rostand. Mabao aliyokuwa akifungwa hasa ya krosi na kona, yalikuwa yakiwachoma sana mashabiki na kila inapokwenda kupigwa kona basi huko jukwaani hawakuwa na furaha kabisa.

Mabosi wakapiga akili na kumshusha kikosini kipa Klause Kindoki, raia wa DR Congo, ambaye wiki zake mbili mazoezini zilitosha kumfanya kuteka nyoyo za mashabiki na kutuliza mizuka kabisa.

Kila shabiki wa Yanga aliyeishuhudia ikiwa kambini pale Morogoro na matizi iliyofanya, amekubali wamepata bonge la kipa kama ilivyo kwa David De Gea wa Manchester United.

Mwanaspoti ambalo lilikuwepo kambini hapo kushuhudia kila kinachoendelea, limefanya mahojiano maalumu na Kindoki, ambaye anafunguka mazito.

Cheki ujio wake Yanga

Safari ya Kindoki kutua Jangwani haikuvuma sana kama ilivyokuwa kwa mastaa wengine kwani, mabosi wa Yanga waliamua kufanya mambo yao kwa siri. Yanga walianza kufanya mazungumzo na meneja wake, ambaye alitua nchini.

Hata hivyo, Kindoki ameondoka wakati klabu yake ya Racing Club de Kinshasa ikiwa bado inahitaji huduma yake kutokana na uwezo mkubwa wa kulinda lango.

“Nimeondoka Racing nikiwa kipa namba moja na nahodha msaidizi, nilikuwa mwisho wa mkataba wangu na mazungumzo ya kuongeza mwingine yalianza, lakini nikapokea ofa ya Yanga na nikaona ni fursa nyingine katika maisha yangu ya soka.Niliwaaga mabosi wangu klabuni lakini, hawakutaka kuamini hadi siku waliponikosa mazoezini,” anasema Kindoki.

Ushindani wa namba

Kwa sasa Yanga ina makipa watatu kikosini kwa Mkongo Mwinyi Zahera, mbali na Kindoki yupo Benno Kakolanya na Ramadhan Kabwili, lakini hilo halijawahi kumtisha kabisa.

“Nafurahi kufanya kazi na makipa wawili walio katika kiwango bora, nafikiri ni suala la kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kuisaidia timu yetu.

“Kuhusu nafasi hilo litaamuliwa na makocha ambao wataona nani anaweza kuanza, lakini kwa nafasi yangu nitafanya kazi kubwa kuanzia mazoezini. Nikipata nafasi jukumu langu ni kuonyesha uwezo uwanjani ili mwalimu aniamini, wachezaji wenzangu, viongozi na mashabiki wafahamu kuwa kuna kipa.

“Sikuja Yanga kukaa benchi bali kucheza ili niweze kukuza kipaji changu, unajua hii ndiyo kazi yangu kubwa hivyo, nitajituma kwa mazoezi binafsi ili niwe bora kumshawishi kocha.

Vipi safu ya ulinzi Yanga

Uwezo mzuri wa kipa unategemea pia safu nzuri ya ulinzi, hapa Kindoki anaeleza jinsi alivyowaona na kuwasoma mabeki wake: “Nimewaona mabeki wetu ni wazuri na wana uwezo mkubwa na hapa ni suala la kushirikiana tu ili kutafuta matokeo bora.

“Changamoto kubwa mwanzoni ilikuwa ni kuwajua majina, lakini sasa nimewajua Kelvin (Yondani) Dante (Andrew Vincent), Juma (Abdul), kuhusu lugha nafikiri katika soka hakuna kujua lugha moja, tutazoeana kupitia mawasiliano ya uwanjani lakini, nimeanza kujifunza Kiswahili.

Akizungumzia uwezo wake katika kukabiliana na mashambulizi ya krosi, Kindoki anasema: “Ili uwe kipa mzuri huwezi kuruhusu mabao ya krosi, kipa bora ni lazima awe na uwezo mkubwa kukabiliana na mashambulizi ya namna hiyo”.

“Nimekuwa naangalia na nimeambiwa hapa kipa wetu wa awali alikuwa anafungwa mpaka kona za moja kwa moja, haitakuwa rahisi kwangu nashukuru mabeki wa Yanga ni wazoefu.

“Ukishakuwa na mabeki wazuri kama hawa ni rahisi kutimiza wajibu wako, muda huu tukiwa kambini nimeutumia vyema kuweza kuzoeana nao.”

Ubora wake kucheza penalti vipi?

Yanga ni moja ya timu inayoteseka inapofika changamoto ya penalti vipi kwa Kindoki yupo vizuri?

“Nimekuja nikiwa kipa na siko hapa kujifunza, nina rekodi nzuri katika kucheza penalti lakini ili uwe bora katika eneo hilo unahitaji utulivu na kumsoma mpigaji.

“Nikiwa golini jambo muhimu ni kujua kuwapanga mabeki wangu kwa kuwa, naiona timu nzima nikifanikiwa kuwapanga ni rahisi kukabiliana na washambuliaji wa aina yoyote,” anasema Kindoki ambaye ni shabiki mkubwa wa muziki wa Fally Ipupa.

Vipi mashabiki Yanga?

“Yanga ina mashabiki wengi wanaoipenda timu yao, tumekuja hapa unaona wanakuja kwa wingi mazoezini na wanatuletea hata matunda hii ni ishara, watu wanapenda timu yao.

Hii kwa wachezaji ina maana kubwa sana kwa shabiki anatoka nyumbani anakuja kuangalia mazoezi akiwa na zawadi kwa wachezaji. Tuna deni kubwa sana kwa mashabiki na kulipa kwake ni kufanya vizuri uwanjani,” anasema.