Kinda wa Gwambina amtia njaa Bocco

Friday November 27 2020
bocco pic

KINDA wa Gwambina FC, Meshack Abraham ameendelea kumtia njaa straika wa Simba na kinara wa mabao Ligi Kuu Bara, John Bocco aliyefunga mabao saba mpaka mzunguko wa 12 ukichezwa huku yeye akifunga sita.

Abraham hakutarajiwa na wengi kuwa atakuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao mpaka mzunguko wa 12, amefunga mabao sita akiwa sawa na mastraika Prince Dube wa Azam na Adam Adam wa JKT Tanzania.

Abraham huenda ataendelea kufunga katika mechi zao zijayo ambapo wataikaribisha Azam kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Gwambina, uliopo Wilaya ya Misungwi jijini Mwanza. 

Akizungumza na Mwanaspoti Online Novemba 27, 2020, Abraham amesema hawazi sana kuwa mfungaji bora bali kikubwa anachopambana ni kuhakikisha timu inaendelea kuwepo kwenye ligi msimu ujao.

Amesema timu yao ni ngeni kwenye ligi hiyo, hivyo akili za wachezaji, benchi la ufundi pamoja na mashabiki ni kuona wanaendelea kuwepo msimu ujao ndio maana kila mmoja anapambana kulingana na majukumu ya nafasi yake.

"Ninachotamani kila mechi ninayopewa nafasi ya kufunga nifunge bao, kwa kufanya hivyo itakuwa msaada kwa timu yangu kupata matokeo mazuri ambayo tunayahitaji ili kufikia malengo ya kubaki kwenye ligi msimu huu,"

Advertisement

"Kama ikitokea nimekuwa mfungaji bora si jambo baya kwangu nitafurahi kwani hakuna mchezaji ambaye hapendi mafanikio kulingana na majukumu ya nafasi yake lakini itakuwa faida hata kwa upande wangu kwani nitajitangaza," amesema Abraham

Advertisement