Kinda Mtibwa aipasua kichwa Azam FC
Muktasari:
- Mbali na Azam, Singida Black Stars nayo imeonyesha nia ya kumtaka beki huyo chipukizi ambaye ameendelea kuonyesha ukomavu mkubwa licha ya umri wake mdogo, jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa karibu kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa.
KLABU ya Azam imeingia rasmi katika mbio za kuwania saini ya nahodha na beki wa kati wa Mtibwa Sugar, Evody Haroun (18), ambaye amekuwa mmoja wa wachezaji vijana wanaofanya vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Mbali na Azam, Singida Black Stars nayo imeonyesha nia ya kumtaka beki huyo chipukizi ambaye ameendelea kuonyesha ukomavu mkubwa licha ya umri wake mdogo, jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa karibu kabla ya dirisha la usajili kufunguliwa.
Taarifa kutoka vyanzo vya karibu na mchezaji huyo zinaeleza kuwa viongozi wa Azam na Singida Black Stars tayari wameanza mawasiliano ya awali na upande wa mchezaji huyo kwa lengo la kujadili uwezekano wa kufanikisha usajili wake mapema.
Evody amekuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Mtibwa Sugar msimu huu, akicheza nafasi ya beki wa kati huku pia akionyesha uwezo mkubwa wa kuongoza timu akiwa amekabidhiwa jukumu la unahodha katika umri mdogo, jambo ambalo limewavutia wengi.
Kocha wa mradi wa Yanga Soccer School, Mohamed Badru anaamini moja ya sifa zinazomtofautisha Evody ni uwezo wake wa kusoma mchezo mapema, kushinda mipira ya juu pamoja na utulivu wake akiwa na mpira miguuni, hali inayomfanya kuwa beki wa kisasa anayehitajika na timu nyingi.
"Nimemuona ana kitu kikubwa sana, anahitaji kupata timu ambayo itamuendeleza kama ataondoka Mtibwa Sugar kwangu ni kati ya wachezaji bora wa baadaye na kwa pale alipo ni sehemu nzuri sana," alisema.
Inaelezwa kuwa Azam inaona usajili wa mchezaji huyo kama sehemu ya mkakati wa kuendelea kujenga kikosi chenye mchanganyiko wa vijana na wachezaji wenye uzoefu huku ikitazama kukijenga kikosi hicho kwa mipango ya muda mrefu chini ya kocha Florent Ibenge.
Kwa upande wa Singida Black Stars, viongozi wa klabu hiyo wanatajwa kuvutiwa na uwezo wa Evody kutokana na mpango wao wa kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Licha ya uwepo wa hilo, Mtibwa Sugar inaelezwa kutokuwa tayari kumuachia kirahisi mchezaji huyo muhimu, hasa kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya kikosi na nafasi yake kama mmoja wa viongozi wa timu.
Hadi sasa mazungumzo hayo bado yako katika hatua za mwanzo na hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa huku kila upande ukiendelea kutathmini masharti mbalimbali yatakayohusika katika dili hilo.