Kilichowaponza JKT, UDSM DBL ni hiki hapa

Muktasari:
- Ligi hiyo ambayo kwa sasa imesimama kupisha mashindano ya Kombe la Taifa, imekuwa na ushindani mkubwa tofauti na miaka iliyopita.
Kujiamini kwa JKT na UDSM Outsiders, ndiko kulikofanya hadi timu hizo zikapoteza michezo yao miwili ya Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL).
Ligi hiyo ambayo kwa sasa imesimama kupisha mashindano ya Kombe la Taifa, imekuwa na ushindani mkubwa tofauti na miaka iliyopita.
JKT iliyokuwa ikijiamini itashinda, ilifungwa na UDSM iliyoondokewa na nyota wake kama Evance David, Troyne Edward, Mwalimu Heri waliojiunga na Stein Warriors, Jimmy Brown na Baraka Sabibi na JKT.
Hata hivyo, UDSM ilisajili nyota wapya wenye uwezo mkubwa na walioipa ushindi dhidi ya JKT wa pointi 60-56.
KIUT iliifunga JKT kwa pointi 84-74, katika mchezo uliowashangaza wengi kutokana na uchanga wa timu hiyo.
KIUT pia iliifunga UDSM kwa pointi 64-53, kabla ya kufungwa na Pazi 63-50 mchezo wa pili.
Wakati huo huo, timu kongwe ya Savio iliyowahi kuwa bingwa 2016, 2017, 2018 na 2021 nayo ilizinduka baada ya kupoteza michezo minne.
Ilifungwa na DB Oratory kwa pointi 75-66, Stein Warriors pointi 93-74, Vijana City Bulls pointi 70- 50, Dar City pointi 92-73
Baadaye ikaifunga Polisi kwa pointi 93-59, Chui 94-79, Kurasini Heat 98-70 na Mgulani JKT 106-39.
Kocha wa timu hiyo, Ally Petar kutoka Temeke, alisema Ligi ya mwaka huu timu yoyote inaweza ikafungwa.
“Nimeona timu zinazoshiriki ligi hiyo zimejiandaa vizuri, ndiyo maana ushindani umekuwa ni mkubwa,” alisema Petar.