Kilichomuua aliyefia uwanjani chatajwa

JUZI vilio na simanzi vilitawala katika kijiji cha Shiwinga wilayani Mbozi mkoani Songwe wakati wa mazishi ya mchezaji yaliyofanyika jana, Belle Mgala aliyefia uwanjani, huku chanzo kikitajwa.

Mgala  aliyekuwa akiitumikia Manchester FC alifikwa na mauti hayo wakati wakicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Super Eagle kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwinga baada ya kuruka juu kufuata mpira uliopigwa na kuwekewa mgongo uliodaiwa ulimfanya aanguke chini.

Mganga Mkuu Msaidizi katika Hospitali ya Mbozi Mission alipopelekwa kwa uchunguzi, Dk Julius Mnkondya amesema baada ya vipimo walibaini marehemu aliangukia kisogo na kufanya ubongo kutikisika.

Dk Mnkondya amesema mara kadhaa mchezaji au mtu yeyote anapodondokea kisogo husababisha ubongo kuathirika ‘Troumatic brain injury’ akiwaomba wachezaji na watu wengine kujenga utaratibu wa kucheki afya mara kwa mara.

“Muda mwingine unakuta mtu alikuwa na magonjwa mengine kama presha, shinikizo la damu au kisukari, hivyo anapopatwa changamoto yoyote tatizo huanzia pale” amesema Dk Mnkondya.

Daktari huyo kitengo cha tiba, ameziomba timu zote nchini kuhakikisha wanakuwa na wataalamu wa afya wenye ujuzi katika mabenchi yao ili kunusuru vifo vya wana michezo.

Kwa upande wake mmoja wa wadau wa soka mkoani humo, Onesmo Mnkondya alisema imekuwa masikitiko makubwa kumpoteza kijana huyo ambaye alikuwa amechaguliwa katika timu ya Mkoa.

“Hata katika mashindano ya MoC Cup alishiriki vyema na tulimchagua kwenye kikosi cha timu ya Mkoa, alikuwa na kipaji cha mpira ila tunashukuru kwa yote kwani ni mapenzi ya Mungu” amesema mdau huyo, huku Emil Minga ameongeza mchezaji huyo alikuwa moja ya wachezaji waliokuwa na vipaji hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa soka la Mkoa wa Songwe.

“Ni masikitikio na huzuni kubwa kwa sisi wadau wa soka, alikuwa mwenye nidhamu na kipaji na ndoto yake bado haikuwa imetimia na tulimtarajia kwa makubwa sana” amesema Minga.