Kikapu Mwanza mwendo wa dozi tu

Muktasari:
- Ligi hiyo iliyoanza Agosti 4, mwaka huu, iliendelea mwisho wa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mirongo jijini Mwanza, Crossover (CIC) iliinyuka Chuo cha Cuhas 78-51, huku nyota wake Bryan Edward akiibuka nyota wa mchezo huo kwa kufunga pointi 30, asisti mbili na rebaundi tano.
TIMU za Crossover (CIC) na Young Profile zimeanza kwa ushindi katika michezo yao ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Mwanza, huku wachezaji Hamis Hamis na Bryan Edward waking’ara na kuibuka nyota wa michezo hiyo kwa kufunga pointi nyingi na kuzibeba timu zao.
Ligi hiyo iliyoanza Agosti 4, mwaka huu, iliendelea mwisho wa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mirongo jijini Mwanza, Crossover (CIC) iliinyuka Chuo cha Cuhas 78-51, huku nyota wake Bryan Edward akiibuka nyota wa mchezo huo kwa kufunga pointi 30, asisti mbili na rebaundi tano.
Katika mchezo wa pili, Young Profile iliichapa Planet 69-63 huku nyota wake, Hamis Hamis akiibuka nyota wa mchezo kwa kufunga pointi 21, pointi tatu mara tano, rebaundi tatu, asisti mbili na kupokonya mipira mara moja.
Katika ligi hiyo ambayo bingwa mtetezi ni Eagles Mwanza, ilifunguliwa Agosti 4, mwaka huu kwa Profile kuinyuka Eagles inashirikisha timu za Crossover, Orotario, Planet, Profile, Cuhas, Eagles Mwanza, Young Profile na Sengerema.
Nahodha wa Oratorio ya Igoma, Edwin Kimbulu, baada ya kuwatazama wapinzani wanaoshiriki ligi hiyo anaamini wana uwezo wa kufanya vizuri na kubeba ubingwa kwani wana kikosi kizuri ambacho ni damu changa na wachezaji wenye uzoefu wa muda mrefu.
“Maandalizi yetu ni mazuri na tuko vyema malengo yetu ni kuwakuza wachezaji vijana kwa sababu tunaamini katika vijana, timu yetu ina mchanganyiko wa wachezaji wachanga na wazoefu na wikendi hii tutacheza mechi yetu ya kwanza dhidi ya Sengerema,”
“Ushindani upo tumetazama michezo yote kuona wapinzani wetu lakini haitatusumbua.”