Kigogo Yanga ala shavu SAZI

Muktasari:

Arafat na wajumbe wenzake wengine walioteuliwa, watakuwa na jukumu la kusaidia maandalizi ya michuano ya Senior Challenge Cup 2024, itakayofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, kuanzia mwishoni mwa Juni.

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, amemteua Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji na Mkurugenzi wa Shirika la Bima kuwa miongoni wa wajumbe wa kusaidia Kamati ya Saidia Zanzibar Ishinde (SAZI).

Waziri Mwita ametangaza uteuzi huo, wakati wa mkutano na wanahabari uliofanyika Migombani, Zanzibar.

Arafat na wajumbe wenzake wengine walioteuliwa, watakuwa na jukumu la kusaidia maandalizi ya michuano ya Senior Challenge Cup 2024, itakayofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, kuanzia mwishoni mwa Juni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waziri huyo, wengine walioteuliwa ni Ayoub Mohammed Mahmoud (mwenyekiti), Said Kassim Marine (katibu), Ussi Salum Pondeza, Nassor Ali Salim Jazira, Fatma Ramadhan Mandoba, Mwalimu Ali Mwalimu, Naima Said Shaame, Ramadhani A Bukini na Abulghafar Idrissa Juma.

Michuano ya Kombe la Chalenji inarejea baada ya kufanyika mara ya mwisho mwaka 2019 wakati Uganda ilipobeba taji kwa kuifunga Eritrea kwa mabao 3-0, huku Kenya ikimaliza ya tatu kwa kuichapa Tanzania Bara kwa mabao 2-1.