Kifo cha Hans Poppe, mahakama yakubali ombi la mawakili wa utetezi

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya kughushi inayowakabili viongozi watatu wa Klabu ya Simba, wameomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuahirisha kesi hiyo, kutokana na Mwenyekiti wa Kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Zacharia HansPope kufariki dunia.

Hans Poppe amefariki dunia Septemba 10, 2021 katika hospitali ya Aga Khan, wakati akipatiwa matibabu baada ya kuugua ugonjwa wa Uviko-19.

Hata hivyo mazishi ya Hans Poppe yanatarajia kufanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.

Hans Poppe na wenzake wawili ambao ni aliyekuwa rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu Kaburu, wanakabiliwa na mashtaka nane yakiweno ya kughushi, matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha bila Kamati ya Utendaji ya Simba,kukaa kikao.

Wakili wa washtakiwa hao, Benedict Ishabakaki na Kung'e Wabeya, wametoa taarifa hiyo, leo Septemba 14, 2021 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya Aveva kuendelea kujitetea, baada ya mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu washtakiwa wote.

Mbali na kuomba mahakama hiyo iahirishwe shauri hilo, pia wamedai tarehe ijayo watawasilisha taarifa rasmi ya msiba wa Hans Poppe ikiwemo cheti cha kifo.

"Mheshimiwa hakimu tunaomba kesi hii uiahirishe hadi tarehe nyingine kwa sababu tuna msiba, lakini tarehe ijayo tutakuja na taarifa rasmi ya msiba wa Hans Poppe ikiwemo cheti cha kifo" amedai Ishabakaki.

Hakimu Mkazi Mkuu anayesikiliza shauri hilo, Thomas Simba, amekubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo kupisha shughuli za mazishi.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 22, 2021 itakapoendelea.

Awali, wakili wa Serikali Mwandamizi, Maghela Ndimbo, ameieleza Mahakama hiyo kuwa shauri hilo limeitwa mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kujitetea.

Hata hivyo kutoka sababu zilizotolewa mawakili wa washtakiwa,  Ndimbo ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na kesi hiyo.

Agosti 31, 2021 kesi hiyo ilishindwa kuendelea kutokana na Hans Poppe kuwa mgonjwa na kushindwa kufika mahakamani hapo kuhudhuria kesi yake.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa nane,, yakiwemo ya  kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila Kamati ya Utendaji ya Simba,kukaa kikao.

Katika mashitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, anadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika mashitaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.