Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kifimbo cha Mfalme kutua nchini siku nne

KIFIMBO Pict

Muktasari:

  • Mbali na kukimbizwa, pia kifimbo hicho ambacho zamani kilifahamika kwa jina la kifimbo cha Malkia, kitachorwa vivutio vya Tanzania na kutangazwa kwenye michezo ijayo ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland.

KIFIMBO cha Mfalme kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa michezo ya Jumuiya ya Madola, kitakimbizwa hapa nchini kwa siku nne kuanzia Agosti 2 hadi 6, 2025.

Mbali na kukimbizwa, pia kifimbo hicho ambacho zamani kilifahamika kwa jina la kifimbo cha Malkia, kitachorwa vivutio vya Tanzania na kutangazwa kwenye michezo ijayo ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland.

Kwa mujibu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid, kifimbo hicho kitakapowasili kitakimbizwa jijini Dar es Salaam na Zanzibar.

Tofauti na miaka ya nyuma, msimu huu kifimbo hicho imeelezwa kitachorwa vivutio vya Tanzania na kitabebwa na wanamichezo wa Tanzania kwenye michezo ijayo ya Madola itakayofanyika Julai 2026, ikishirikisha nchi zaidi ya 70 mwanachama.

“TOC imewapa taarifa Baraza la Michezo Zanzibar na lile la Bara (BMT) juu ya ujio wa kifimbo hicho ambacho zamani kilifahamika kama cha Malkia, baada ya kifo cha Malkia Elizabeth, sasa kinafahamika kama kifimbo cha Mfalme.

“Tunasubiri majibu yao kuhusu maeneo ambako kitakimbizwa, utamaduni wa kifimbo hicho mara zote huwa kinapelekwa Ikulu,” alisema.

Alisema tofauti na kifimbo cha miaka ya nyuma ambacho kilikuwa na GPS na kukimbizwa kwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Madola, msimu huu kitakapowasili nchini, kitabaki hadi kwenye michezo ijayo ya Madola.

“Hapa nchini kitanakishiwa na vivutio vyetu ambavyo tutavipendekeza na wachezaji wetu watakaokwenda kwenye michezo hiyo wataondoka nacho,” alisema.

Katika michezo hiyo, Tanzania ina rekodi ya kufanya vizuri na kutwaa medali kadhaa kupitia riadha huku michezo iliyopita ngumi walitwaa medali mbili za fedha.


OLIMPIKI DAY

Katika hatua nyingine, TOC imezungumzia maadhimisho ya Siku ya Olimpiki (Olympic Day) ambayo kwa hapa nchini yatafanyika Juni 21, 2025.

Makamu wa Rais wa TOC, Henry Tandau, alisema hafla hiyo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani humo.

Amesema mbali na ratiba zingine, kutakuwa na mbio za polepole za kilomita 2.5 kwa watoto na mbio za kilomita 5 ambazo zitaanzia na kumalizikia Uwanja wa Jamhuri, pia kutakuwa na mchezo wa kuvuta kamba.

“Maandalizi yanakwenda vizuri, tunawakaribisha wenyeji wa Dodoma na wageni kutoka mikoa mbalimbali kuja kushiriki siku hii kubwa ya Olimpiki.”