Kiduku anaogopa sindano kuliko ngumi

BINGWA wa Ngumi za Kulipwa anayeshikilia mikanda ya UBO Mabara na ule wa Shirikisho la Masumbwi Tanzania (PST), Twaha Kassim 'Kiduku' amesema amekuwa akiogopa kuchomwa sindano kuliko ngumi za wapinzani anaokutana nao ulingoni.

Kiduku aliyasema hayo baada ya kupimwa afya mkoani Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya pambano la kuwania ubingwa wa WBF jijini Mwanza dhidi ya bondia wa Afrika Kusini, Asemahle Wallem litakalochezwa wikiendi hii na kukiri amekuwa muoga wa kuchomwa sindano mwilini.

Alifafanua uogoa huo umetokana na kupata madhara ya kushindwa kutembea kwa siku nne baada ya kuchomwa sindano akiwa na umri wa miaka 10 hali iliyopelekea zoezi hilo la kumpimwa afya lisimame kwa dakika kadhaa akibembelezwa kupimwa afya na daktari na timu yake.

Kiduku alisema akiwa na umri wa miaka 10 ya utoto wake alichomwa sindano na kushindwa kutembea kwa siku nne hali inayomfanya akumbuke tukio hilo na kushindwa kutoka akilini mwake na kutengeneza uoga uliodumu hadi sasa.

“Nafikiri kabla ya hapo nilikuwa siogopi kuchomwa sindano japo watoto wengi wana asili ya kuogopa kuchomwa sindano, ila nilichomwa sindano nikiwa na umri wa miaka 10 na kushindwa kutembea kwa siku nne baada ya hapo nimekuwa nimekuwa muoga kuchomwa sindano kwa sababu lile tukio bado halijafutika katika akili yangu hiyo ndio sababu ya kuwa muoga,” alisema Kiduku.

Kiduku alisema linapokuja suala la kupima afya inayohusu kutolewa damu kwa njia yoyote ile amekuwa akiogopa tofauti na damu inayotoka wakati wa kusukumiana makonde mazito usoni na mpinzani wakiwa ulingoni kwa sababu haoni tabu kwa sababu naye anaumiza na kuumizwa.

Pambano lake dhidi ya Msauzi litakuwa la raundi 10 katika uzito wa kilo 76 na yupo fiti baada ya kujifua katika kambi ya Vijana Social Sabasaba Manispaa ya Morogoro.

Kocha wa bondia huyo, Power Iranda alisema amemuandaa bondia wake kwa kumtreni katika nyanja tatu za kupata ushindi.

“Tumemnoa Kiduku katika maeneo matatu ya kushinda, kupandana na kupiga ngumi za akili na mpinzani akibadilika ulingoni atakavyokuja kama atatumia nguvu tumemtreni Kiduku kutumia akili na akitumia akili atatumia akili na nguvu ili kumdhibiti mpinzani wake  na kupata ushindi.