Kibu: Tulieni muone mambo!

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujiwinda na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City na jana asubuhi ilicheza mechi ya kirafiki na Cambiaso na kuifunga mabao 3-2, huku mshambuliaji wao kinara wa mabao, Kibu Denis akitupia mawili na akiwatuliza mashabiki wa klabu hiyo.
Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena, uliopo Bunju pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam na bao jingine la Msimbazi liliwekwa kimiani na Sadio Kanoute, huku Simon Msuva anayejishikiza kwa sasa Cambiaso Academy akiifungia timu hiyo yote mawili.
Mara baada ya mchezo huo, Kibu aliliambia Mwanaspoti, mabao hayo mawili licha ya kuwa ni katika mechi ya kirafiki, lakini yanampa faraja kwa kuamini anavuka malengo aliyojiwekea kabla ya kutua Msimbazi akitokea Mbeya City mwanzoni mwa msimu huu.
Kibu alisema wakati anasajiliwa na Simba alikuwa alijiwekea malengo ya kuisaidia timu kufanya vizuri na kufunga idadi ya mabao saba ambayo alimaliza nayo msimu uliopita akiwa na Mbeya City na hadi sasa ameshayafikia na huku ligi ikisaliwa na mechi tano za kufungia msimu huu.
“Tumebakiwa na mechi tano kabla ya msimu kuisha nataka kupambana na kupewa nafasi ya kucheza ili kuongeza idadi ya mabao niliyofunga sasa na hilo naimani linawezekana,” alisema Kibu na aliongeza;
“Unajua nikiendelea kufunga timu yangu itakuwa inafanya vizuri kwenye mechi zilizobaki na kupata ushindi kama ambavyo tunahitaji katika michezo iliyobaki, hivyo mashabiki wa Simba watulie kila kitu kitaenda sawa, kwani kama wachezaji tuna morali ya kumaliza kwa heshima.”
Kibu anatarajiwa kukutana na chama lake la zamani, Mbeya City Alhamisi katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku Msimbazi ikiwa na deni la kuipigo cha bao 1-0 ilichopewa ugenini.