Kibu D, namba na hali halisi vinapotofautiana

Muktasari:

  • Wiki iliyopita ilikuwa ya Kibu Dennis. Sijajua ukweli hadi sasa. Tulichosikia ni hajataka kusaini mkataba mpya pale Msimbazi na anataka kuondoka zake pindi msimu huu utakapofikia tamati. Dau ambalo anatajwa kulikataa ni kubwa kama vile dau ambalo linatajwa kumshawishi kwenda kwingineko.

SIJUI kama tutajua tufuate lipi katika soka la kisasa. Takwimu au macho yetu? Tangu tuanze kushika kompyuta zetu soka limeanza kutuchanganya. Tuamini katika lipi kati ya tunachokiona kwa macho au takwimu.

Wiki iliyopita ilikuwa ya Kibu Dennis. Sijajua ukweli hadi sasa. Tulichosikia ni hajataka kusaini mkataba mpya pale Msimbazi na anataka kuondoka zake pindi msimu huu utakapofikia tamati. Dau ambalo anatajwa kulikataa ni kubwa kama vile dau ambalo linatajwa kumshawishi kwenda kwingineko.

Ghafla kuna mkanganyiko wa hisia kutoka kwa wachambuzi na mashabiki mbalimbali wa soka kuhusu Kibu. Anastahili zaidi ya Sh300 milioni? Hili ndio swali. Msimu huu amefunga bao moja tu katika ligi kuu huku Simba wakihangaika kuisaka nafasi ya pili inayokaliwa na Azam. Tayari Yanga wanaonekana kuwa mabingwa.

Licha ya kufunga bao moja lakini Simba wanaona umuhimu mkubwa wa Kibu. Hapa ndipo unapoibuka mjadala wa takwimu dhidi ya hali halisi. Takwimu zinatuonyesha Kevin De Bruyne ni bora kuliko Zinedine Zidane. Macho yetu yanatuambia Zidane ni bora kwa mbali kuliko staa huyu wa Manchester City na timu ya taifa ya Ubelgiji.

Takwimu zinatuonyesha Cristiano Ronaldo ni bora kuliko Diego Maradona na Ronaldo De Lima. Hali halisi inatuambia hao wawili ni bora kuliko Ronaldo. Hapa ndipo linapoibuka suala la Kibu. Hana mabao mengi lakini kuna kitu ambacho Simba wanakiona kwa Kibu kuliko kwa wachezaji wengine.

Ukiwaambia Simba nani aondoke kati ya Kibu au Freddy Michael watakwambia Freddy aondoke ingawa ni huyu huyu amefunga mabao mengi kuliko Kibu. Soka la namba linatuchanganya katika dunia ya kisasa. Unajaribu kushindana na hali halisi. Hapa ndipo Kibu anapohitaji pesa nyingi katika mkataba wake. Hapo ndipo Kibu anadengua.

Kibu anawapa Simba nguvu. Ana mwendo, nguvu, anajaribu kupambana akiwa na mpira na hata asipokuwa na mpira. Ukiwa kocha lazima umpende Kibu. Ukiwa kiongozi lazima umpende Kibu. Ukiwa shabiki lazima umpende Kibu. Tatizo linakuja pale utakapoangalia namba zake. Hapa ndipo utakapoamua mwenyewe kama umpe mkataba mnono au hapana.

Inanikumbusha Yannick Bangala katika msimu wake wa kwanza Yanga. Alichaguliwa kuwa mchezajj bora wa msimu. Namba zilikataa kabisa. Alifunga bao moja. Hatukuwa na hesabu za namba nyingine kama pasi na mengineyo lakini tulichoshuhudia ni alikuwa mchezaji bora uwanjani. Hakukuwa na manung’uniko hata kutoka kwa watani kuhoji kwa nini Bangala alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu.

Wanaohoji kwa nini Kibu atake pesa nyingi, wanaangalia namba na wana hoja. Wanaoamini Kibu anastahili kuitingisha Simba wanaangalia hali halisi uwanjani na wana hoja ya kusikilizwa. Wanaitazama Simba vyema na kuona walau ni mmoja kati ya wachezaji ambao wanaipa timu uhai mkubwa uwanjani.

Lakini kwa nini tumefika hapa? Kuna mambo mawili au matatu. Jambo la kwanza ni kukubali ukweli kadri timu inavyoondoka katika makali yake ndivyo ambavyo wachezaji kama Kibu wanaweza kuishikilia timu mateka. Labda ile Simba ya Clatous Chama, Jose Luis Miquissone, Larry Bwalya, Chris Mugalu, John Bocco, Meddie Kagere na Hassan Dilunga huenda Kibu asingeonekana kama mchezaji anayeweza kuidengulia timu.

Kwa Simba hii inayokosea kusajili kila kukicha kwa nini Kibu asiringe? Ni mwendelezo ule ule wa Chama. Tofauti ni Chama anadengua wakati msimu unaendelea wakati Kibu anadengua mwishoni mwa msimu. Unaitazama timu inavyocheza unapima umuhimu wako na kugundua ni mkubwa katika timu. Hapo ndipo unapoanza kuhangaisha watu. Kwa mfano, Kibu alikuwa nchini wakati Miquissone akiwa katika moto wake. Leo Miquissone amerudi na amekuwa mchezaji wa kawaida tu anayeburuzwa na Kibu katika benchi. Kwa nini Kibu asiringe? Hadi yeye achoke uwanjani ndio Miquissone aingie. Kwa nini Kibu asitake pesa nyingi mwishoni mwa msimu?

Ukiwa na wachezaji wengi wakali kikosini umuhimu wa wachezaji unapungua kidogo. Wanaweza kujifunza kwa watani zao namna ambavyo kwa ukatili kabisa waliamua kuachana na Bangala pamoja na Djuma Shaban. Ni kutokana na umuhimu wa wachezaji wengi katika kikosi. Ndio maana hadi leo wanasonga mbele kwa mafanikio zaidi kuliko hapo awali.

Lakini kuna jambo jingine ambalo mabosi wetu wa soka inabidi wajifunze, hasa pale Msimbazi. Wachezaji wengi muhimu mikataba yao imebakiza wiki chache tu. Kwa nini wanaruhusu mikataba ya wachezaji ifike tamati kisha waanze kusumbuka kukimbizana nao wasaini mikataba mipya? Mara zote wachezaji wanapewa mikataba ya miaka miwili.

Nadhani kitu sahihi ni kumwongeza mchezaji mkataba pindi anapomaliza mwaka wake wa kwanza tu.

Labda klabu zinaona ni kujiweka katika hatari kwa sababu kiwango cha mchezaji kinaweza kushuka lakini ukweli, mwishowe, mambo kama haya ya Kibu ndio huwa yanaibuka na kuiweka timu katika mazingira magumu. Sio Kibu peke yake. Sadio Kanoute anamaliza mkataba. Chama anamaliza mkataba.

Wakati mwingine naamini viongozi wanakuwa bize zaidi kusajili wachezaji wapya klabuni kuliko kuangalia namna gani wataweza kuwabakiza wachezaji mastaa klabuni. Mwishowe jambo kama hili la Kibu huibuka katika nyakati tete huku klabu ikikosa nguvu kwa mchezaji kwa sababu baada ya siku chache mchezaji anakuwa huru.

Tusubiri na kuona suala la Kibu litaishia wapi lakini kwa ninavyotazama kwa nje ni mchezaji ambaye Simba wanamhitaji. Tayari nafahamu kuna wachezaji wengi Simba hawatakuwepo msimu ujao na hii ni hatari. Unahitaji kubakisha wachezaji kadhaa ambao wataungana na wapya ili timu isiwe mpya kabisa.

Zaidi ni baada ya kubadili uraia wake Kibu anachukuliwa ni mchezaji mzawa. Katika hizi klabu zetu imeanza kuwa nadra kuwa na wachezaji wazawa ambao wanaanza katika kikosi cha kwanza. Inawasaidia viongozi katika mchakato wa kutafuta wachezaji wa kigeni. Inapunguza mawazo kwa viongozi kutafuta kundi kubwa la wageni klabuni.

Hata kama Kibu ataondoka Simba na kutua Azam au Yanga bado viongozi wa klabu hizo watakuwa wamepata faida kwa sababu wataendelea kuzilinda nafasi za wageni klabuni.

Mara nyingi viongozi huwa wanachanganyikiwa katika nafasi za wachezaji wa kigeni. Huwa wanaziona chache kutokana na kushuka kwa viwango vya wachezaji wazawa.