KenGold sherehe za Ligi Kuu zimeanza

‘ANZENI kushona suti’. Ni neno alilotamka Kocha Mkuu wa Ken Gold, Jumanne Challe akielezea safari yao ya matumaini ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao, huku akisaka pointi tatu tu kati ya mechi nne zilizobaki kumaliza Championship.

Ken Gold ndio wanaongoza ligi hiyo kwa pointi 60 na wamebakiza mechi nne wakianzia jijini Arusha dhidi ya TMA na Mbuni kisha kurejea Sokoine kukamilisha ligi kwa Polisi Tanzania na FGA Talents.

Timu hiyo ya wilayani Chunya mkoani Mbeya inashiriki Championship kwa msimu wa nne sasa na mwaka huu wamedhamiria kufanya kweli kutimiza ndoto hiyo.

Kimahesabu Ken Gold inayo nafasi kubwa ya kupanda daraja kutokana na pointi ilizowaacha walio chini yao Pamba Jiji wenye alama 55 na kama itashinda mechi mbili itajihakikishia kupanda.

Akizungumza na Mwanaspoti, Challe alisema haoni kinachoweza kuwazuia msimu ujao kuvaa jezi ya Ligi Kuu, akitamba kuwa wanaoshona suti waendelee kwani wamejipanga.

Alisema katika michezo iliyobaki bila kuangalia wapinzani wao wa chini wanasaka alama tano pekee, akieleza iwapo wangeshinda dhidi ya Pamba sherehe zingeanza kikosini.

“Huu msimu ni wetu kwenda Ligi Kuu, anayeshona suti aendelee, tunahitaji alama tano lakini kama walio chini yetu wakikwama popote pointi zitapungua, kimsingi tumedhamiria” alisema Challe.

Kocha huyo hakusita kukiri mchezo dhidi ya Pamba kuwapa ugumu akieleza walihitaji kulipa kisasi lakini walishindwa hadi kujikuta wakiondoka na sare ya 2-2.

“Mechi ya kwanza tulipoteza 2-1 tukaahidi kulipa kisasi lakini tumeshindwa ila hata pointi moja si haba kwani imetuongezea kitu, tunajipanga mechi zijazo” alisema Kocha huyo.