Kaze: Tulitarajia kutanguliwa kufungwa, Mubiru amjia juu refa

Mbeya. Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze amesema kutanguliwa mabao matatu dhidi ya Mbeya City ilitokana na uchovu wa vijana wake, huku akielezea sababu ya kuwaanzisha nyota ambao hawakuwa na namba kikosini.

Leo Yanga iliwaanzisha baadhi ya wachezaji ambao hawakuwa na namba tangu kuanza msimu huu akiwamo kipa Erick Johola, Mamadou Doumbia ambaye ni mechi yake ya tatu, Chrispin Ngushi, Dickson Ambundo, Denis Nkane na David Bryson.

Baadaye benchi la ufundi la timu hiyo lilifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Jesus Moloko, Benard Morrison na Tuisila Kisinda na kufanya mechi kuchangamka.

Hata hivyo Moloko alijikuta akishindwa kumaliza dakika 90 kwa kuoneshwa nyekundu na straika wa Mbeya Nassoro Machezo baada ya kuzipiga uwanjani na mwamuzi Tatu Malobo.

Katika mchezo wa leo, City ikianza kwa kasi ilitangulia kupata mabao matatu yaliyofungwa na George Sangija na Richardson Ngy'ondya aliyefunga mawili.

Hata hivyo Yaga walisawazisha mabao hayo kupitia kwa Benard Morrison aliyetupia mawili ikiwamo moja ya penalti, Salum Aboubabakari 'Sure Boy' na kawaacha midomo wazi mashabiki wa City wasiamini kilichotokea.

Kaze amesema uchovu na kutofanya mazoezi ndio kiliwapa wakati mgumu dakika 45 za kwanza na kwamba walitarajia kutokea kitu hicho.

Amefafanua kuwa hata hivyo kuwa na wachezaji wenye uzoefu ambao walianzia benchi wameweza kumaliza mchezo na kwamba hiyo ilikuwa ni mbinu za kiufundi kuwaanzisha wachezaji ambao hawakuwa na nafasi katika mechi zilizopita.

"Yote ilikuwa ni mbinu za kiufundi ila tuwapongeze wachezaji kwa kazi nzuri waliyofanya japokuwa tulihitaji kushinda, tunaamini mechi ijayo tutakuwa tofauti kwakuwa tutapata muda wa kutulia na kujiandaa" amesema Kaze.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Mbeya City, Abdalah Mubiru amesema mpira ni saikolojia na kwamba waliharibiwa na mwamuzi wa mchezo huo akisema amewanyima penalti.

Amesema kwa sasa wanaenda kujipanga upya na mechi ijayo dhidi ya KMC ili kusubiri hatma yao kubaki au vinginevyo.

"Mpira ni saikolojia, kuna maamuzi hayakuwa mazuri kwa refa, mmeona ziko penalti ametunyima za wazi ila tunaenda kujipanga na mechi ijayo ambayo itakuwa ya mwisho kujua hatma yetu" amesema Mubiru.