Kaze apangua safu ya ushambuliaji Yanga

Muktasari:

Yanga inacheza katika Uwanja wa CCM Kirumba ikiwafuata wenyeji wao KMC katika mchezo wa kwanza wa ugenini wa kocha wao mpya Cedric Kaze.

Kocha Mkuu wa Yanga amefanya mabadiliko matatu katika kikosi chake wakiwafuata KMC akipangua safu ya ushambuliaji yake.

Kwenye kikosi ambacho Kaze amepanga kuanza nacho amewaanzisha mshambuliaji Michael Sarpong ambaye katika mchezo uliopita wa nyumbani aliingia kipindi cha pili akitokea benchi lakini pia amemuanzisha kwa mara ya kwanza mshambuliaji mwingine mzawa Waziri Junior.

Mchezo uliopita kocha huyo alimuanzisha Yacouba Sogne ambaye leo ataanzia benchi  akibadilishana na Sarpong.

Kiungo Deus Kaseke naye amepata nafasi ya kwanza ya kuanza katika utawala wa Kaze akichukua nafasi ya Haruna Niyonzima ambaye leo ataanzia benchi na atacheza winga ya kulia na Tuisila Kisinda atacheza ya kushoto.

Kiungo mwenye mabao mengi katika kikosi hicho Mukoko Tonombe mwenye mabao mawili ameendelea kupata nafasi sambamba na Feisal Salum 'Fei Toto'.

Hata hivyo Kaze hajaigusa kwa lolote safu yake ya ulinzi akiendelea kuwaamini kipa Metacha Mnata, beki wa kulia Kibwana Shomari, beki wa kushoto Yassin Mustapha na mabeki wa kati nahodha Lamine Moro na msaidizi wake Bakari Mwamnyeto.

Safu hiyo ya ulinzi imeonyesha umakini mkubwa ambapo mpaka sasa imefikisha dakika 450 sawa na mechi tano bila kuruhusu bao.

Mwenye benchi Kaze amewapa nafasi Kipa Farouk Shikhalo, beki Abdallah Shaibu 'Ninja', kiungo Zawadi Mauya, Niyonzima, Farid Mussa ambaye alikuwa nyota wa mchezo katika timu hiyo akichaguliwa na mashabiki wa timu hiyo akianzia benchi, Yacouba na Ditram Nchimbi.

 

HALI ILIVYO UWANJANI

Yanga imekuwa ya kwanza kutinga uwanjani saa 8:17 mchana, huku kukitanguliwa na gari la usalama na kupokelewa na makomando wao getini.

 

Wakati timu hiyo ikiingia uwanjani, mashabiki waliokuwa katika mlango kuingia vyumbani, waliamsha shangwe wakati wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi wakishuka kwenye gari.

 

Hata hivyo, Mwanaspoti Online imeshuhudia baadhi ya viongozi wa KMC, wakiongozwa na Afisa Habari wake Christina Mwagala wakiwahi mapema uwanjani.

 

KMC wao waliwasili dakika 10 baadaye kimyakimya bila shangwe na kwenda moja kwa moja katika vyumba vya kubadilishia nguo.