Katwila apewa mmoja Geita Gold
Muktasari:
- Katwila ambaye amewahi kuzifundisha Mtibwa Sugar, Mbeya City na Tanzania Prisons, atasaidiwa na Paul Nonga ambaye pia atakuwa kocha wa viungo pamoja na Agustino Malindi akiwa kocha wa makipa.
Geita Gold imempa mkataba wa mwaka mmoja, Zuberi Katwila kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo kwa msimu ujao wa Ligi ya Championship.
Katwila ambaye amewahi kuzifundisha Mtibwa Sugar, Mbeya City na Tanzania Prisons, atasaidiwa na Paul Nonga ambaye pia atakuwa kocha wa viungo pamoja na Agustino Malindi akiwa kocha wa makipa.
Katwila anachukua mikoba iliyoachwa na Mohamed Muya ambaye aliondolewa baada ya msimu uliopita kumalizika na timu hiyo kushindwa kupanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara kutokana na kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ya Championship.
“Geita Gold inajivunia kumkaribisha Kocha Zuberi Katwila kama nahodha mpya wa benchi la ufundi,” ilisomeka taarifa ya Geita Gold na kuongeza.
“Anakuja na falsafa mpya, mbinu za ushindi, na kiu isiyo na kipimo ya mafanikio. Msimu huu si wa kawaida ni wa kupindua meza.”
Akizungumzia ujio huo wa Katwila, Ofisa Habari wa Geita Gold, Samwel Dida alisema hatua hiyo ni sehemu ya mipango ya klabu hiyo ya kupanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja baada ya kukwama msimu uliopita.
“Katwila amesaini msimu mmoja, atasaidiwa na Paul Nonga kama msaidizi na kocha wa utimamu wa mwili (Fitness) na kocha wa makipa ni Agustino Malindi,” alisema Dida na kuongeza.
“Mipango ya klabu msimu huu ni kupanda Ligi Kuu moja kwa moja.”
Dida amesema mbali na benchi la ufundi, wamefanya maboresho ya kikosi ikiwemo kuwabakiza nyota muhimu akiwemo Yusuph Mhilu, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Fredy Sululu.
“Tumefanya maboresho makubwa katika baadhi ya maeneo kuanzia utawala na kikosi ili kuongeza ufanisi ndani ya timu,” alisema Dida.