Karia mgombea pekee urais, kuthibitishwa na mkutano mkuu

Wallace Karia sasa atathibitishwa na mkutano mkuu kuendelea kuwa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kwenye uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo utakaofanyika Agosti 7 mjini Tanga.

Karia amebaki peke yake katika kinyang'anyiro hicho katika kiti cha urais baada ya wagombea, Hawa Mninga na Evans Mgeusa kuondolewa kwenye usaili.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Benjamin Karume alisema Mgeusa na Mniga wameondolewa kwa kutokidhi baadhi ya vigezo vya kikanuni ikiwamo uzoefu.

Amesema Karia sasa atakuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo ambaye hatapigiwa kura na badala yake mkutano mkuu utampitisha kwa mujibu wa kanuni.

"Kanuni mpya kwa muktadha wa makabrasha ambayo ninayo, mgombea ambaye atakuwa peke yake hatapigiwa kura.

"Tofauti na chaguzi zilizopita ambapo walipigiwa kura za ndiyo au hapana, kwenye uchaguzi huu itakuwa ni tofauti kutokana na mabadiliko ambayo mkutano mkuu ulifanya hivyo nafasi yoyote yenye mgombea mmoja wanampitisha," amesema na kuongeza.

"Na kumpitisha kwenyewe sio kwa kupigiwa kura bali kutokana na katiba kanuni inasema atathibitishwa kwa sababu tayari alishapata udhamini ambao unaonyesha tayari mgombea umekubalika.

Alipoulizwa kuhusu kanuni hizo,  Karume amesema kanuni zimeelezea tu kwamba wanampitisha kwa kutokana na yaliyojiri kwa kanuni namba fulani ambayo itawauliza wajumbe wa mkutano mkuu kama wanamthibitisha.

Hata hivyo amesema, wagombea walioenguliwa kwenye usaili wana nafasi ya kukata rufaa kuanzia Julai 11 hadi 13.