Kambi Simba yazidi kunoga, kocha mpya kutua wiki hii Misri

KABLA ya wiki hii kumalizika katika kambi ya Simba kocha mpya wa viungo, Mtunisia Karim Sbai atawasili kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo, Ismailia Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
Kikosi cha Simba kilianza maandalizi ya msimu ujao Julai 15, katika viwanja vilivyopo kwenye hoteli waliyofikia na kwa siku wanafanya awamu mbili asubuhi na jioni ili kuhakikisha miili ya wachezaji inakuwa sawa.
Leo Jumatatu mazoezi awamu ya kwanza yalikuwa ya nguvu na yalifanyika katika (Gym), iliyopo ndani ya jengo hilo kisha jioni watakwenda kufanya yale ya uwanjani.
Tangu kuanza kwa mazoezi hayo Simba yalikuwa yakisimamiwa na kocha mkuu, Zoran Maki akisaidiwa na msaidizi wake, Selemani Matola.
Zoran amesema limekuwa jambo jema kwao benchi la ufundi kuongezewa Sbai kwani ni moja ya makocha aliyowahi kufanya nae kazi siku nyingi kabla ya kujiunga na kikosi cha Simba.
Amesema ndani ya siku mbili hizi Sbai atajiunga nao na haraka kuanza kazi ya maandalizi kwa kuwapatia wachezaji mazoezi muhimu kwani kipindi cha pre-season ni moja ya eneo lake la msingi katika kazi kwani mazoezi mengi huwa ya kuaandaa miili ya wachezaji.
"Naimani uwepo wa Sbai kuna kitu kitakuwa kimeongezeka katika benchi letu la ufundi," amesema Zoran na kuongeza;
"Uzuri mwingine wa Sbai mbali ya taaluma hiyo ya ukocha wa viungo ni mzuri kwenye kufanya kazi ya usaidizi kwa kushirikiana na Matola naimani tutakuwa na benchi la ufundi imara zaidi."