Kama utani wamechemsha

KUNA wakati mwingine upepo unakuwa mbaya kwa mastaa wa soka kutokana na sababu mbalimbali, hivyo kusababisha kushindwa kukonga nyoyo za mashabiki wao.
Ni kama ilivyotokea kwa wachezaji waliosajiliwa kwa mbwebwe katika dirisha dogo la usajili msimu huu kutokana na kuonyesha viwango vikubwa walikotoka, lakini wameshindwa kuendelea kudhihirisha ubora wao katika timu zao mpya.
Wachezaji kama Denis Nkane wa Yanga aliyesajiliwa kutoka Biashara United, Crispin Ngushi aliyetoka Mbeya Kwanza na Chico Ushindi aliyesajili na timu hiyo kutoka TP Mazembe.
Wakati Nkane akisajiliwa na Yanga akitokea Biashara United alikuwa na mabao mawili na kiwango bora, lakini ameshindwa kuendeleza ubora wake kutokana na ushindani mkubwa aliokutana nao kwenye kikosi cha Jangwani ambako pia akipangwa amekuwa akikosa mabao mengi licha ya umachachari wake uwanjani.
Kwa upande wa Ngushi ambapo wakati anasajiliwa kutoka Mbeya Kwanza alikuwa na mabao matatu, lakini ndani ya kikosi cha Yanga ameshindwa kupata nafasi kabisa kwani hata mechi ambazo amekuwa akipangwa ameshindwa kuonyesha ubora wa kumshawishi kocha Nasreedin Nabi kuendelea kumwamini kama ilivyo kwa Chico ambaye wakati anasajiliwa na Yanga mashabiki walikuwa na matumaini makubwa kwake, lakini hadi sasa hana bao lolote na hana nafasi kikosi cha kwanza.
Baadhi ya wachezaji wengine ambao walisajiliwa na timu zao kwenye dirisha dogo lakini hadi sasa hawajaonyesha makali ni Clatous Chama wa Simba, Ibrahim Ajibu, Shaaban Chilunda na Yahya Zayd wa Azam, Ditram Nchimbi (Geita Gold), Habib Kiyombo na Eliuter Mpepo wa Mbeya Kwanza.
Ajibu alikuwa hana namba katika kikosi cha Simba na kutimkia Azam, na wengi walitegemea atafanya makubwa katika klabu yake mpya, lakini mambo yamekuwa tofauti kwani amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara wakati Chilunda amekuwa akipata nafasi, lakini ameshindwa kuonyesha kiwango na kushindwa kuibeba timu yake katika baadhi ya mechi ikiwemo ile ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Coastal Uniona ambayo alikosa mabao mengi.
Kwa upande wa Chama aliyerejea Simba akitokea RS RS Berkane ya Morocco alikocheza nusu msimu, lakini hadi sasa bado hajakonga nyoyo za mashabiki wa klabu hiyo na hayupo kwenye ubora ambao wengi wameuzoea kutoka katika miguu yake.
Chama mwenye mabao manne kwenye ASFC na matatu kwenye ligi hivi sasa ni majeruhi, hivyo amekosa baadhi ya michezo ya timu yake.
HAWA HAPA WAKONGWE
Akiwazungumzia wachezaji hao winga wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema wengi hasa wa timu kubwa hawakufanya kilichotarajiwa mpaka kufikia kusajiliwa kwenye dirisha dogo.
“Wengi hawajaonyesha viwango bora sijui sababu ni nini, ila kikubwa ni wao wenyewe watambue unaposajiliwa kuna kitu watu wamekiona kwako, hivyo ni lazima upambane kuonyesha na kuwa msaada kwa timu na usipofanya hivyo unakuwa umewaangusha waliokusajili na hata mashabiki,” alisema.
“Licha ya wengi wao kutopata nafasi, lakini hata wakiingizwa kutoka benchi kipindi cha pili hawaonyeshi ubora labda kidogo yule Nkane anajitahidi, japo bado anatakiwa kupambana.” Kocha mzoefu, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema: ‘Ujue usajili wa dirisha dogo hupati kitu unachohitaji kwa mchezaji tofauti na unapomsajili mwanzoni kabisa mwa msimu. Dirisha dogo mchezaji anaingia kwenye ushindani moja kwa moja hadi apate muunganiko na wenzake inachukua muda na ndio jambo ambalo naona wachezaji hao linawagharimu lakini muhimu wazidi kupambana.”