Kama hamkuwaelewa Tambwe na Ngoma, kwa Kegere msitoke kapa

JULAI 10, mwaka 2013 Simba ilimpokea usiku wa manani, straika kutoka Burundi. Alikuwa ametoka kwenye michuano ya Kombe la Kagame 2013 iliyochezwa kule Sudan. Tanzania ilishindwa kutuma wawakilishi wao, Simba na Yanga waliouchuna kwa kisingizio cha kuhofia machafuko ya nchi hiyo. Hata Kenya na Sudan Kusini ambao walikuwa wanaanza kuingizwa CECAFA baada ya kujitenga na Sudan nao waliyachunia fainali za mwaka huo.
Yanga walipaswa kwenda kama watetezi na Simba kama mabingwa wa Tanzania kipindi hicho. Pengine hii ndio iliyowapa nafasi Vital'O kutamba, kwani kwa miaka miwili mfululizo taji lilikuwa likishikiliwa na Yanga.
Kwani mnadhani alikuwa nani? Ni huyu Amissi Tambwe aliyekuwa ametoka kuisaidia Vital'O ya kwao Burundi kubeba taji la kwanza la michuano hiyo.
Straika huyo aliibuka Mfungaji Bora kwa mabao sita, huku akitua Msimbazi msimu huo akitoka kubeba pia tuzo ya Mfungaji Bora wa misimu miwili mfululizo katika Ligi Kuu ya Burundi.
Wapo waliombeza wakati anatua, lakini jamaa kwa msimu wake wa kwanza tu alitupia kambani mabao 19 na kunyakua Kiatu cha Dhahabu, huku asilimia kubwa ya mabao yake yakiwa ya kichwa.
Simba walipompata Dan Sserunkuma waliamua kumpotezea Mrundi huyo, Yanga wakamdaka akaendelea kufanya yake nusu msimu aliifungia mabao 13 na msimu uliofuata akabeba tena Kiatu cha Dhahabu kwa mabao 21.
Mbali na umahiri wake wa kufunga, lakini kama alivyokuwa Simba, Tambwe aliweka rekodi ya kupiga hat trick mfululizo na mpaka leo anashukilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye ha hatrick nyingi katika Ligi Kuu Bara akiwa na kama sita.
Lakini wakati Tambwe akifanya yake, Yanga ilishusha mashine nyingine matata ambayo iliifanya Yanga iwe mwiba mkali mbele akishirikiana na Tambwe na Simon Msuva. Donald Ngoma alikuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani. Jamaa alikuwa anajua kufunga, kumiliki mpira, mbio na nguvu mbali na kujiamini kwake kwa kutoogopa mabeki kiasi cha kuwaponza kulimwa kadi nyekundu kwa rafu walizokuwa wakimchezea kama njia ya kumdhibiti.
Tambwe na Ngoma walizimika kwa kuwa walikuwa majeruhi kwa muda mrefu, lakini msimu uliopita, Emmanuel Okwi aliendelea kuthibitisha kuwa, yeye ni mfalme katika soka la Tanzania licha ya kutokea Uganda.
Nyota hao wote wa kigeni walikuwa kama wanatoa darasa kwa wachezaji wa ndani hasa wanaocheza safu ya ushambuliaji. Msuva, John Bocco, Mbaraka Yusuf na wengine walikuwa wakuifundishwa jinsi ya kutupia kambani.
Nyota hao wa kigeni walikuwa wakifunga kwa kichwa, miguu yote na kujua kujipanga mbele ya mabeki na lango la adui na kuwaadhibu wakifanya uzembe.
Okwi kwa sasa hajaanza makeke katika Ligi Kuu, Tambwe na Ngoma bado vilevile, lakini kuna jamaa anaitwa Meddie Kagere. Katika mechi mbili tu ya Simba amedhirisha ndiye mwalimu mpya ambao wazawa wanapaswa kujifunza kwake.
Ukiyaangalia mabao mawili aliyoyafunga dhidi ya Mbeya City, ndio utajua jamaa ni mchezaji wa aina gani na mshambuliaji mwenye jukumu la kufunga anatakiwa awe vipi. Achana na kejeli kwamba ni mzee, Kagere anajua kufunga na kama mabeki wa timu pinzani hawatakuwa makini wataumbuliwa sana kama walivyoumbuliwa mabeki wa Mbeya City na kipa wao, Owen Chaima.
Wachezaji wachache wenye ujasiri wa kuingiza kichwa kwenye nafasi ya mguu wa beki. Kagere kaweza. Mchezaji gani mzawa wa nafasi hiyo anaweza kufanya hivyo? Adama Salamba? Hapana. Marcel Kaheza, Mohammed Rashid, Yohana Mkomola ama Ibrahim Ajibu? Hapana! Labda Bocco, mmoja ya mstraika asilia wa Tanzania waliopo kwa sasa.
Tangu wameondoka kina Emmanuel Gabriel, Joseph Kaniki, Monja Liseki, Mohammed Hussein 'Mmachinga' kwa kizazi cha karibuni ambao watoto wa dot.com wanawafahamu nani mwingine unayeweza kumlinganisha na Bocco? Labda Shaaban Idd Chilunda unaweza kumlinganisha naye kwani alimudu kuvaa viatu vyake alivyoviacha pale Chamazi.
Ila kuna kila sababu ya mastraika wa timu zetu ambao wakicheza mechi moja na kufunga, wanapiga sana kelele, eti ndio nimeanza kazi. Kisha inapita mechi 10 hata bao la kuotea wanashindwa kutupia nyavuni, ili likataliwe tu na mwamuzi.
Kama nyota wetu walishindwa kuambulia kitu kwa Tambwe, Ngoma, Obrey Chirwa na Okwi, basi kwa Kagere wasitoke kapa wamwangalie Mnyarwanda huyo anawazidi kitu gani, ili kula naye sahani moja kama walivyokuwa wakifanya kina Msuva, Elias Maguli na Jeremiah Juma walipokuwa wakikimbizana na Tambwe.
Ama Bocco alivyokuwa akienda sambamba na Okwi ndani ya Wekundu wa Msimbazi katika msimu uliopita.
Ila kama wataendelea kulala, basi wajue kabisa Kagere na nyota wengine wa kigeni watawaburuza sana kwa vile hawataki kujifunza, ila kulalamika tu wakiwekwa benchi na makocha wa timu zao, wakati hawana maajabu uwanjani.