Kalambo aanika kilichomkwamisha

Muktasari:
- Nyota huyo alijiunga na Coastal Union siku ya mwisho ya dirisha la usajili kufungwa Januari 15, 2025, baada ya kuachana na Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, ingawa hadi sasa hajacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara na timu hiyo.
KIPA wa Coastal Union, Aaron Kalambo amesema sababu kubwa ya kutocheza kwa muda mrefu akiwa na kikosi hicho msimu huu, ni kutokana na kuandamwa na majeraha ya goti kwa muda mrefu, hali iliyomfanya kutoonekana kama alivyotarajia mwanzoni.
Nyota huyo alijiunga na Coastal Union siku ya mwisho ya dirisha la usajili kufungwa Januari 15, 2025, baada ya kuachana na Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, ingawa hadi sasa hajacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara na timu hiyo.
“Msimu umekuwa mgumu kwangu kwa sababu sikutarajia kama ningekutana na changamoto hii, wakati najiunga na Coastal kiukweli niliona malengo yangu ya kucheza Ligi Kuu yametimia, ingawa majeraha ya mara kwa mara yameniharibia,” alisema.
Kipa huyo wa zamani wa Dodoma Jiji, alisema ni ngumu kuonyesha ushindani kwa mechi mbili za Ligi Kuu zilizosalia msimu huu, hivyo kwa sasa anahesabu malengo yake yamekwama na anaangalia jinsi atakavyojipanga tena upya kurudisha ubora wake.
“Nilisaini mkataba wa miezi sita hivyo, msimu ukiisha nitakuwa huru, siwezi kusema kama nitaongeza mwingine au lah! kwa sababu sijafanya uamuzi wa mwisho, siku zilizobakia lolote linaweza kutokea pia,” alisema.